LUIS Jose Miquisson Alipokuja kwa mara ya kwanza nchini walimuita Konde Boy. Alipewa jina hilo kwa sababu mbili. Kwa ubora wake kufananishwa na msanii Harmonize. Lakini kwa asili yake kuwa Msumbiji ambako kuna Wamakonde, pia historia inavyotufumba midomo kwa Miquissone.
Akadumu Simba kwa mwaka mmoja akiwa katika kiwango bora. Aliwatetemesha mabeki nchini. Ilikuwa ngumu kumkaba Miquissone. Alikuwa na kasi ya ajabu, uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kufunga.
Akiwa pamoja na Clatous Chama waliifanya Simba kuwa tishio kwenye mechi za Ligi Kuu na mashindano ya CAF. Nani amesahau lile bao maridadi alilowafunga Al Ahly kwa Mkapa? Hakuna. Alikuwa wa moto kwelikweli.
Kiwango hicho ndicho kilisababisha anunuliwe na mabingwa wa Afrika, Al Ahly. Ndiyo kiwango kilichosababisha Simba ipate zaidi ya Sh2 bilioni katika mauzo yake. Ilikuwa ni historia mpya katika mauzo ya wachezaji nchini.
Ndiyo historia hii imefanya Simba imrejeshe tena. Wanakumbuka namna miguu yake ya dhahabu ilivyowabeba. Ndio sababu mashabiki wengi walifurahia kurejea kwake Msimbazi.
Nini kimetokea? Huyu Miquissone aliyerudi siye yule aliyeondoka. Ni kama vile alibadilishwa pale Uwanja wa Ndege.
Miquissone huyu hana kasi tena. Hana utulivu tena mbele ya lango. Ni kama vile amesahau soka.
Mwanzo tuliamini kwa kuwa alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu labda anahitaji kupata muda wa kucheza ili kurejea katika ubora wake. Bahati mbaya sasa inakwenda miezi mitano na zaidi na bado Miquissone amekuwa vilevile. Hana maajabu.
Yaani leo Kibu Denis amekuwa hatari kuliko Miquissone. Saido Ntibazonkiza katika ‘uzee’ wake anacheza vizuri kuliko Miquissone. Nini kimemkuta Konde Boy? Inasikitisha sana.
Ila ni kitu cha kawaida katika soka. Wapo wachezaji wengi mahiri waliohama klabu moja kwenda nyingine ikawa ndio mwisho wao. Mifano ni mingi sana.
Wengi wanakumbuka kilichomkuta Fernando Torres wakati amehama Liverpool kwenda Chelsea. Hakuwahi kuupata ubora wake tena.
Nini kilimkuta Eden Hazard alipokwenda Real Madrid akitokea Chelsea? Ni ngumu kusimulia. Hazard alitoka Chelsea akiwa ndiye nyota wa timu lakini alipofika Madrid akawa kichekesho. Hakuweza kufika katika kilele cha ubora wake tena.
Ni kama ilivyokuwa kwa Phillipe Coutinho alipohamia Barcelona akitokea Liverpool. Aliondoka akiwa shujaa Anfield, lakini kule Barcelona hakuwa na maajabu. Wakasubiri ubora wake hadi wakachoka na kuamua kuachana naye.
Kwa hapa Bongo, Yanga iliwakuta kwa Heritier Makambo na Tuisila Kisinda. Waliondoka wakiwa wa moto. Makambo aliuzwa kwenda Horoya na Kisinda kwenda RS Berkane na Yanga ikavuta mkwanja wa maana.
Baada ya kurejea kwa mara ya pili hawakuwa na jipya. Makambo alikosa ushawishi mbele ya Fiston Mayele. Kisinda hakuwa na madhara tena. Hakuwa na utulivu tena mbele ya lango. Baada ya muda Yanga ikaachana nao wote wawili.
Ndiyo soka. Kuna wakati wachezaji mahiri hupoteza ubora wao pindi wanapohama timu moja kwenda nyingine. Historia hufanya mashabiki kutamani wacheze tena katika timu zao, lakini mambo huwa yanagoma.
Kuna baadhi ya wachezaji wachache huwa wakiondoka bado wanarudi wakiwa na moto wao. Ni kama ilivyokuwa kwa Emanuel Okwi. Kila alipoondoka Simba na kurejea, makali yake yalikuwa vile vile. Okwi hakuwahi kushuka kiwango. Ndiyo sababu Simba ilimrejesha kila wakati.
Kwa Miquissone wana Simba wanaweza kuendelea kusubiri kidogo, lakini kama mambo yatakwenda hivi hadi mwisho wa msimu huenda wakaamua kuachana naye.