Ummy Mwalimu Agoma Kujiuzulu Sakata la Wajawazito Kujifungulia Sakafuni

 

Ummy Mwalimu Agoma Kujiuzulu Sakata la Wajawazito Kujifungulia Sakafuni

Baada ya baadhi ya watu kumtaka Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ajiuzulu kuonesha uwajibikaji kufuatia madai ya baadhi ya wajawazito kujifungulia kwenye sakafu katika Kituo cha Afya cha Buzuruga, jijini Mwanza, kiongozi huyo amesema hatorudi nyuma huku akidai  tukio hilo ni kampeni chafu dhidi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).


Ummy ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Disemba 2023, kupitia ukurasa wake wa Twitter muda mfupi baada ya madai hayo kuibuliwa katika mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watu wakimtaka ajiuzulu wakidai ameshindwa kusimamia vyema sekta ya afya.


“Mwisho niseme kuwa mimi na timu yangu hatutakatishwa tamaa na kampeni chafu zinazoendeshwa mara kwa mara na baadhi ya watu. Ndiyo uongozi, kiongozi unahitaji kuwa na ngozi ngumu, muhimu ni kuwa na dhamira njema na kubwa zaidi kumtanguliza Mungu mbele yeye ndiye muweza wa kila kitu,” ameandika Ummy.


Kauli hiyo ameitoa wakati akitolea ufafanuzi sakata hilo, ambapo amedai taarifa zilizosambazwa ni za upotoshaji.


Aidha, Ummy amekiri kuwa sekta ya afya ni kubwa hivyo changamoto haziwezi kukosekana na kwamba ataendelea kuchapa kazi na kujituma usiku na mchana kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote


“Aidha, nitaendelea kupokea na kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazohusu huduma za afya nchini kupitia jukwaa hili na majukwaa mengine. Pia, hatutasita kutoa ufafanuzi wa hoja pale tunapoona kuna upotoshaji,” ameandika Ummy.


Ummy amesema katika kipindi cha uongozi wake sekta ya afya imepata mafanikio makubwa huku akiahidi kuendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya kwa watanzania.


Kauli hiyo ya Umma imekuja ikiwa ni siku moja tangu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, jijini Mwanza, Wakili Kiomoni Kibamba, kukanusha uwepo wa tukio hilo akidai hakuna mjamzito anayejifungulia chini katika kituo cha afya cha Buzuruga.


Taarifa ya Wakili Kibamba ilisema, awali kituo hicho kilikuwa na vitanda vitatu kwa ajili ya kujifungulia kitendo kilicholeta changamoto hivyo Serikali iliongeza hadi kufikia sita.


“Hivyo kwa maelezo hayo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inapenda kuuhakikishia umma kuwa katika Kituo cha Afya cha Buzuruga, hakuna wakina mama wanaojifungulia chini kama taarifa ya mtandaoni inavyoeleza,” imesema taarifa ya Wakili Kibamba.


Kuhusu picha iliyosambaa mitandaoni, taarifa ya Wakili Kibamba imesema sio ya hivi karibuni kama inavyodaiwa, bali ilipigwa Septemba 2022.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad