Dar es Salaam. Mamlaka Hali ya Hewa nchini (TMA), imetoa taarifa ya utabiri wa hali ya hewa eneo la Katesh wilayani Hanang Mkoa wa Manyara ukionyesha kuwa kutakuwa na mvua za wastani kwa siku mbili mfululizo kuanzia leo.
Akitoa utabiri huo leo Desemba 8, 2023 Meneja Utabiri wa mamlaka hiyo, Dk Mafuru Kantamla amesema kuanzia leo hadi kesho Desemba 9, 2023 mvua za wastani zitanyesha wilayani humo.
Dk Kantamla amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza leo Desemba 8, 2023 saa 12 jioni hadi saa 6 usiku, ambapo zitakuwa za wastani, mawingu kiasi na upepo wa wastani unaofikia kilomita 20 hadi 30 kwa saa, huku joto nyuzi likiwa kati ya 25C na 15C.
Kwa kesho Desemba 9, 2023, Dk Kantamla amesema mvua hizo zitaanza saa 9 alasiri hadi saa 6 usiku, zikiandamana na mawingu kiasi huku upepo ukitarajiwa kuvuma kwa kilomita 20 hadi 30 kwa saa na joto litakuwa kati ya nyuzi joto 25C na 15C.
"Huu utabiri unaonyesha mvua zinazotarajia kunyesha maeneo ya Wilaya ya Hanang, zitakuwa ni za kawaida sana," amesema Dk Kantamla.