Mwanza. Ni pigo. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya familia mbili zinazoishi Mtaa wa Mabatini Kaskazini jijini Mwanza kupoteza watoto wawili ambao ni wanafunzi baada ya kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu.
Wakati wawili wakifariki, watu wengine saba katika familia hizo, wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure.
Tukio hilo lilitokea Alhamisi ya Desemba 11 mwaka huu, baada ya familia hizo kununua uyoga uliyokuwa ukiuzwa na mfanyabiashara (jina halijatambulika) katika mtaa huo.
Siku moja baada ya kula chakula hicho, watu tisa walianza kutapika na kuharisha mfululizo, jambo lililoibua hofu na sintofahamu kwa ndugu, jamaa ma marafiki.
Mkazi wa mtaa huo, Eva Jonas, aliyefiwa na mtoto wake wa pili, Thompson Jonas (18), amesema siku hiyo baada ya kutoka katika shughuli zake za kuuza genge, alikutana na mfanyabiashara huyo akiuza uyoga, huku watu wengine wakinunua na ndipo naye aliponunua wa Sh1,000 na alipofika nyumbani aliandaa mlo wa usiku (ugali na uyoga).
“Kesho yake saa 7 mchana, Thompson alianza kuhisi maumivu ya tumbi, kisha akaanza kutapika na kuharisha. Mimi pia nikaanza kutokewa na hiyo hali na watoto pia,” amesema Eva na kuongeza;
"Nikishirikiana na jirani yangu, nilijikaza tukawachukua watoto kuwapeleka zahanati ya Mabatini shuleni ambako tulitakiwa kwenda kituo cha afya Buzuruga kutokana na hali zetu," amesema.
Walipofikishwa kituo cha afya Buzuruga walipatiwa huduma ya kwanza na kufanyiwa vipimo, daktari alimweleza kuwa dalili zinaonyesha wamekula chakula chenye sumu, huku akielezwa kuwa ini la mwanaye limeanza kubadilika kutokana na chakula hicho.
Baada ya kulazwa siku tatu, juzi Jumapili saa 4:30 asubuhi ndipo mwanaye alifariki dunia.
Eva amesema kifo cha Thompson kimeacha kovu ambalo halitasahaulika, kwani alikuwa akisubiri matokeo baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mabatini, Novemba mwaka huu.
Amesema Thompson alikuwa mtoto pekee katika uzao wake aliyehitimu, jambo linalomfanya kuwa tegemezi kwa familia yake baada ya mumewe kufariki dunia zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Simulizi ya Edna, haitofautiani na ya Mwalikwa Zuberi, ambaye mtoto wake wa kike, Warda Zuberi (10), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Victoria Hope iliyopo Nyegezi jijini Mwanza kufariki dunia.
Katika familia yake, Zuberi amesema mbali na binti yake kufariki, bibi wa marehemu, Maua Ibrahim (78) anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Bugando baada ya kula uyoga huo.
“Siku hiyo binti yangu alikuja kumsalimia bibi yake, ndipo alipokuta amenunua uyoga ambao baada ya kuupika, baadhi ya ndugu na watoto waliokuwepo walikataa kuula kwa sababu ulikuwa na ladha mbaya,” amesema Zuberi.
Alisema baada ya wengine kususia chakula hicho, Maua na mjukuu wake walikula ndipo walipopatwa na madhara kwa kuanza kuharisha na kutapika.
“Warda alifariki dunia akipatiwa matibabu Bugando baada ya madaktari kusema hana madhara kwenye ini wala kongosho, lakini figo zake zimepunguza uwezo wa kuchuja taka kwenye mkojo,” amesema Zuberi. Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mabatini Kaskazini, Hilda Massawe aliyekutwa na Mwananchi akihani msiba wa Thompson, alisema uyoga huo umeacha pigo katika mtaa wao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure jijini humo, Dk Bahati Msaki alipopigiwa simu kujua hali za waathiriwa wa chakula hicho, amesema anafuatilia suala hilo huku akiahidi kutoa majibu. Alipopigiwa tena jana saa 9:20 alasiri, simu yake iliita bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo, huku akisema jeshi hilo limeanza msako wa kumtafuta mfanyabiashara huyo aliyekuwa akiuza uyoga huo.