Mwimbaji wa Bongofleva, Vanessa Mdee a.k.a Vee Money, 35, anafurahia miaka minne ya kutokunywa pombe kabisa, anasema ni moja ya maamuzi bora aliyowahi kuchukua katika maisha yake.
Kauli ya Vanessa inakuja takribani miezi saba tangu Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kutangaza kuwa ameachana na matumizi ya pombe tangu Januari mwaka huu, kwa lengo la kulinda afya yake ya mwili na akili.
Wakati Vee na Wema wanafikia uamuzi huo, Shirika la Afya Duniani (WHO), linabainisha kuwa matumizi mabaya ya pombe husababisha vifo milioni 3 kila mwaka, ikiwa ni asilimia 5.3 ya vifo vyote ulimwenguni, huku yakisababisha magonjwa zaidi ya 200.
Husababisha vifo na ulemavu mapema maishani, katika kundi la watu wenye umri wa miaka 20 hadi 39, takribani asilimia 13.5 ya vifo vyote husababishwa na pombe ambayo pia huchagiza aina za matatizo ya kiakili, kitabia na kiuchumi.
"Sijapata kunywa kinywaji chenye kileo kwa takribani miaka minne, moja wapo ya maamuzi bora zaidi ambayo nimewahi kufanya, asante Mungu kwa neema yako," ameandika Vanessa kupitia Insta Story.
Kipindi Vanessa anatangaza kuachana na muziki, moja ya sababu alizotaja hadi kufikia uamuzi huo ni kuwa muziki ulimpa msongo wa mawazo baada ya kushindwa kufikia matarajio yake, kitu kilichomtumbukiza katika unywaji wa pombe kupita kiasi.
Vee alisema mama yake mzazi alihuzunika sana baada ya kupata habari kuwa ni mlevi, kwa kifupi alipoteza tumaini. Ndipo akaachana na Bongofleva akiwa ametoa albamu moja, ‘Money Mondays’ (2018).
Kwa sasa Vanessa anaishi huko Georgia, Marekani na mchumba wake, Rotimi ambaye alimvisha pete mnamo Desemba 2020, wawili hao kwa mara ya kwanza walikutana Julai 2019 katika tamasha la Essance nchini humo ambapo wote walitumbuiza.
Tayari Vanessa na Rotimi wamejaliwa watoto wawili, Seven (2021) na Imani (2023) ambao hivi karibuni wameonyesha nyuso zao kwenye mitandao ya kijamii kwa mara ya kwanza. Kwa mujibu Vee, Rotimi anapenda sana watoto kwa sababu kwao alizaliwa peke yake, hakuwa na wa kucheza naye.