Msanii wa Bongofleva, Rayvanny hivi karibuni ameachia video ya wimbo wake ‘Mwambieni’ akimshirikisha Mac Voice ambaye kamsaini katika lebo yake, Next Level Music (NLM) tangu Septemba 2021 akiwa ni msanii wa kwanza.
Kwa ujumla huu ni wimbo wa tano kwa wawili hao kushirikiana ndani ya miaka miwili, nyimbo nyingine ni Tamu (2021), Bora Peke Yangu (2021), Pombe (2021) na Muongeze (2022).
Mac Voice ni msanii wa pili kufanya kolabo nyingi na Rayvanny baada ya Diamond Platnumz, Vanny Boy na Chibu wameshirikiana katika nyimbo tisa ambazo ni Salome, Iyena, Mwanza, Tetema, Timua Vumbi, Amaboko, Woza, Ni-tongoze na Yaya.
Kwa upande mwingine, video ya wimbo ‘Mwambieni’ ni rekodi nyingine upande wa penzi la Rayvanny na mpenzi wake Fahyma ambaye amekuwa pamoja tangu mwaka 2015 na kujaliwa mtoto mmoja wa kiume, Jaydan.
Utakumbuka Fahyma au Fahyvanny ni mwanamitindo akiwa ameshinda tuzo za Scream Awards (Nigeria), Starqt Awards (Afrika Kusini), Zikomo Awards (Zambia), Swahili Fashion Week Awards (Tanzania) n.k.
Fahyma ndiye mrembo aliyetokea katika video ya wimbo huo, Mwambieni, hii ni video ya tatu kwa wapendanao hao kufanya pamoja ndani ya mwaka huu na kwa ujumla wameshafanya video sita kwa miaka saba waliyokuwa pamoja.
Hadi sasa Fahyma ameonekana katika video za nyimbo za Rayvanny kama Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).
Na mrembo huyo hajawahi kutokea katika video ya msanii mwingine yeyote yule zaidi ya Rayvanny, alisema fedha anayolipwa na msanii huyo ni nyingi kiasi kwamba hawezi kuchukua kazi ya mwingine. Ndiyo, analipwa kutokana hiyo ni biashara sasa na sio tena mapenzi. Kwa ujumla Fahyma ndiye mrembo aliyetokea mara nyingi zaidi katika video za staa huyo wa NLM, utakumbuka kipindi Rayvanny akiwa na Paula alimtumia katika video ya wimbo wake, Wana-weweseka (2021) na hadi wanaachana ni hiyo moja tu walifanya pamoja.
Hata hivyo, kitendo cha Rayvanny kumtumia Fahyma katika video zake kwa mwaka huu pekee kinatafsiriwa kama kushindana na Marioo ambaye sasa ana uhusiano na Paula, binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani.
Marioo aliyeanzisha uhusiano na Paula baada ya kuachana na Rayvanny, naye kwa mwaka huu tu amemtumia mrembo huyo katika video za nyimbo zake tatu ambazo ni Lonely, Tomorrow na Sing.
Utakumbuka tangu Marioo amekuwa na Paula hajafanya video na mrembo mwingine yeyote yule na video hizo tatu zilitoka kwa kufuatana ndani ya kipindi cha takribani miezi miwili hadi Agosti mwaka huu.
Hivyo alichofanya Rayvanny hivi karibuni ni kusawazisha matokeo kabla ya mwaka haujaisha baada ya mwenzake kum-tangulia, na sasa matokeo yanasoma; Rayvanny 3-3 Marioo, huku Fahyma na Paula wakiwa ndio waamuzi wa mta-nange huo.
Mastaa hao ambao wameshirikiana katika nyimbo mbili, Te Quiero na Anisamehe, ukaribu wao unaonekana kupungua sana, mapenzi yanatajwa kuwa sababu.
Iliwahi kuelezwa Rayvanny hakupenda Marioo kumchukua Paula ingawa alikanusha jambo hilo na kudai wapo sawa.
Kitendo cha Marioo na Rayvanny kujirusha sana na wapenzi wao katika video zao, wanaungana na Diamond na Har-monize ambao nao wamefanya hivyo kwa zaidi ya mara tatu ila sio kwa mfululizo, huku wakiwa na warembo mbalim-bali.
Karibia warembo wote ambao Diamond wamewahi kuwa nao katika uhusiano ameshafanya nao video za nyimbo zake, alianza na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu aliyetokea kwenye video ya wimbo wake, Moyo Wangu (2011).
Naye Hamisa Mobetto ambaye uhusiano wake na Diamond ulikuwa wa siri hadi walipojaliwa mtoto, Dylan (2017), ali-inogesha vizuri video ya ngoma ya Chibu, Salome (2016) akimshirikisha Rayvanny.
Kwa upande wa Zari The Bosslady kama alivyojaliwa watoto wawili na Diamond, Tiffah (2015) Nillan (2016), yeye ame-tokea video mbili za nyimbo za Diamond, Utanipenda (2015) na Iyena (2018) na ndiye mpenzi pekee wa Diamond ali-yefanya naye video nyingi.
Ukija kwa Harmonize, kipindi penzi lake na Jacqueline Wolper lipo katika kilele cha mafanikio yake, walisafiri hadi Afrika Kusini kufanya video ya wimbo, Niambie (2017).
Aliyekuwa mke wa Harmonize, Sarah kutokea Italia waliyedumu katika ndoa takribani mwaka mmoja (2019 - 2020), ametokea kwenye video za nyimbo mbili za Harmonize, My Boo Remix (2019) na Niteke (2019).
Kwa upande wa Kajala Masanja ambaye alivishwa hadi pete ya uchumba na Harmonize, ame-tokea kwenye video moja, Nitaubeba (2022) na muda mfupi baada ya video hiyo kutoka wakaachana.
Na hii ni moja ya video za Harmonize zilizopata mapokezi makubwa ndani ya muda mfupi, hadi sasa ikiwa na ‘views’ zaidi ya 19 milioni YouTube.