Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali imepeleka wataalamu wa miamba ambao watatoa taarifa ya nini kilichotokea na nini kifanyike katika mlima wa Hanang ambao kutokana na maporomoko ya mlima huo, watu zaidi ya 47 wamefariki dunia na kusababisha majeruhi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea)
Mhagama ametoa kauli hiyo leo Jumatatu baada ya kutembelea Kijiji cha Gendabi – Hanang akiwa ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, pamoja na Wakuu wa Vyombo vya ulinzi na Usalama.
Viongozi hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga wamefika katika Kijiji cha Gendabi ambalo ni eneo lililoathirika na maporomoko ya matope kutoka Mlima wa Hanang yaliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 3 Disemba 2023.
Akiwa eneo la tukio hilo, Mhagama, amewaomba wananchi hao kupokea pole ambazo zinatoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliagiza lazima kufika eneo la tukio na kuona nini kifanyike kwa dharura kuhusu uokoaji pamoja na makazi kwa waathirika hao.
“Mambo haya yakitokea kuna mambo ya haraka yanatakiwa yafanyike kwa dharura hivyo tumekuja na kushauriana namna ya kujipanga kwa pamoja ili kufanikisha jambo hilo kwa uharaka” ameongeza Mhagama.
Ameongeza kuwa, maelekezo ya Rais Samia kwanza kuona namna gani tunaweza kuendelea kuokoa watu na kazi hiyo wanaendelea nayo vikosi vya uokoaji, pia kuangalia namna gani ya kuweza kuwasitiri wenzetu waliotangulia mbele ya haki.
Kwa upande wake Bashungwa amesema kazi ya kufungua miundombinu ya barabara inaendelea ili kurahisia kazi za uokoaji na kufikisha huduma muhimu za kijamii katika meneo yaliyoathirika.
Amesema Wakala wa Barabara nchini ( TANROADS) tayari wamefungua barabara ya Singida-Babati ambayo awali ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa tope na magogo ya miti kutoka milimani.