WHO yatoa angalizo mafua makali, Uviko19 vikiongezeka


WHO yatoa angalizo mafua makali, Uviko19 vikiongezeka


Dar es Salaam. Zaidi ya wagonjwa wapya 500,000 wa Uviko- 19 na zaidi ya vifo vipya 2,400 vimeripotiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutokea katika kipindi cha siku 28 zilizopita, Tanzania ikiwemo.

Nchi 104 zimetajwa kuathirika zaidi ya Uviko19, huku homa kali ya mafua inayoambukiza maarufu Influenza ambayo huathiri mapafu na kusababisha watu kulazwa hospitalini ikiongezeka katika baadhi ya nchi.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya nchini Tanzania Desemba 3 kupitia kitengo cha Epidemiolojia na Usimamizi wa Magonjwa, katika sampuli 246 zilizochukuliwa kati ya Novemba 27 na Desemba 3, 2023 waliokutwa na Influenza walikuwa 31 na 33 wengine walikutwa na maambukizi ya Uviko19.

Kutokana na ufuatiliaji wa maeneo mbalimbali kuanzia wiki ya kwanza hadi ya 48 kwa mwaka 2023, umeonyesha maambukizi yalianza kupanda katika wiki ya 45 mpaka 48.


Hata hivyo, jedwali hilo lilionyesha kupanda zaidi kwa Uviko19 ikilinganishwa na influenza kwa mujibu wa namba za sampuli zilizopimwa maabara.

“Duniani kote, katika kipindi cha siku 28 kuanzia Oktoba 23 hadi Novemba 19 2023, nchi 104 ziliripoti kesi za Uviko 19 na nchi 43 ziliripoti vifo vya Uviko19.

“Kumbuka kwamba hii haionyeshi idadi halisi ya nchi ambazo matukio au vifo vinatokea, kwa kuwa nchi kadhaa zimeacha au kubadilisha mara kwa mara kuripoti,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.


Amesema kutokana na takwimu zilizopo, mitindo ya idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa na vifo inapaswa kufasiriwa kwa tahadhari kutokana na kupungua kwa upimaji na mfuatano, sambamba na ucheleweshaji wa kuripoti katika nchi nyingi.

Hata hivyo, amesisitiza nchi kujikita katika kutoa elimu ya kujikinga na Uviko19 pomoja na influenza ili kuzuia maambukizi kuenea zaidi.

Amesema katika kipindi hicho, nchi 62 na 37 zilitoa zilitoa takwimu kuhusu kulazwa hospitalini kwa wagonjwa wa Uviko19 na kulazwa kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) angalau mara moja.

“Kutokana na takwimu zilizopo, zaidi ya watu 84,000 waliolazwa hospitalini na zaidi ya 700 waliolazwa katika ICU waliripotiwa katika kipindi cha siku 28 cha kuripoti.


“Hata hivyo, miongoni mwa nchi zinazoripoti takwimu hizi kwa mfululizo katika vipindi viwili vya kuripoti, kulikuwa na ongezeko la asilimia 26 la wagonjwa wapya wa ICU,” amesema Dk Tedros.

Tangu kuzuka kwa Uviko19 mwaka 2019 nchini China, hadi kufikia Novemba 19, 2023 takwimu za WHO zinaonyesha zaidi ya watu milioni 772 walithibitishwa kupata virusi vya ugonjwa huo unaoathiri mapafu na vifo zaidi ya milioni sita vimeripotiwa ulimwenguni kote.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad