Yanga na Msuva Mambo Safi, Kumtangaza Rasmi Mapinduzi Cup

 

Yanga na Msuva Mambo Safi, Kumtangaza Rasmi Mapinduzi Cup

Hatima ya winga wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Simon Msuva, kurejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga huenda ikajulikana kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kuanza kesho Visiwani Zanzibar, huku nyota huyo akisema lolote linaweza kutokea. Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Msuva ameshaachana na JS Kablie ya Algeria, na sasa yuko huru kujiunga na klabu nyingine.


Uamuzi wa kutangaza usajili wa nyota huyo huko Zanzibar ulitolewa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ambaye pia alikariri klabu yake itamtambulisha mchezaji ambaye si mgeni hapa nchini katika mechi yao ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.


Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema tayari wameshakamilisha mazungumzo na nyota huyo ambaye yuko nchini akifanya mazoezi na kikosi cha Taifa Stars na kinachosubiriwa ni wakati huo sahihi waliopanga.


"Tulitaka kutangaza mchezaji mpya, lakini tumeahirisha, Rais wa klabu akashauri kuwa ni bora tukamtangaze kwenye Kombe la Mapinduzi, mchezo wetu wa kwanza tutamtambulisha mchezaji ambaye tumemwongeza dirisha dogo.


Wasifu wa mchezaji huyo si mgeni sana masikioni mwa watu, hata tukimtangaza kila mmoja atakuwa anamfahamu, ni zawadi kwa Wazanzibar watambue kuna 'chuma' tunakwenda kukishusha, mchezaji bora wa viwango vya juu," alisema Kamwe.


Alisema winga huyo ambaye aliwahi kuichezea pia Wydad Casablanca ya Morocco na Al-Qadsiah FC ya Saudi Arabia anakuja kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni anayetarajiwa kupelekwa katika timu nyingine kwa mkopo au kuvunja mkataba wake.


"Huyo straika anakuja kuchukua nafasi ya Konkoni ambaye kama si kumtoa kwa mkopo basi tutasitisha kabisa mkataba, tuachane naye kwa wema.


Kocha Gamondi (Miguel), ametuambia usajili mkubwa utafanyika dirisha kubwa msimu utakapomalizika," alisema Kamwe.


Msuva alikiri Yanga inafanya mazungumzo naye lakini hakuna muafaka wowote ambao umefikiwa kwa sababu anafahamu Gamondi hana shida na winga na mahitaji yake ni kupata mshambuliaji.


Msuva alisema hata hivyo yeye kazi yake ni kucheza mpira na lolote linaweza kutokea kutokana na uzoefu mkubwa alionao katika kazi yake.


"Yanga ni moja ya timu kubwa, lakini niseme tu nimepokea ofa nyingi, bado ninatamani kuendelea kucheza soka nje ya Tanzania. Hata hivyo lolote linaweza kutokea," alisema Msuva.


Kwa upande wa Gamondi alisema ameshaweka wazi anahitaji kuboresha safu ya ushambuliaji ili kufikia malengo yake katika msimu huu unaoendelea.


“Kuna timu nyingi zinahitaji mshambuliaji, Madrid wanahitaji hata Barcelona wanae Lewandowski (Robert), lakini bado wanahitaji mshambuliaji. Yanga inahitaji hata tukiongeza mmoja itabidi na yeye apewe muda na sio kuingia na kuanza kucheza mechi ya kwanza mnataka afunge mabao matatu.


Hapana kila mchezaji anahitaji muda kuzoea ligi na wakati mwingine tamaduni za nchi alizotoka na Tanzania ni tofauti, kuna muda lugha inakuwa inampa shida wachezaji wengi sana," Gamondi aliongeza.


Wakati huo huo, beki wa kulia wa Yanga, Kouassi Yao, raia wa Ivory Coast anaongoza kwa kutoa pasi za mwisho wa ufungaji, 'assist' kwa upande wa mabeki katika Ligi Kuu Tanzania Bara.


Kwa mujibu wa takwimu za Ligi Kuu, Kouassi, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast ana 'assist' tano mpaka sasa, akifuatiwa na beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda mwenye 'assist' nne.


Wachezaji Paschal Msindo wa Azam FC, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' wote wa Simba wana 'assist' tatu kila mmoja huku mabeki wengine, Cheikh Sidibe (Azam ), David Brayson (JKT Tanzania) na Miraji Abdallah na Coastal Union kila mmoja ana 'assist' mbili.


Kikosi cha Yanga kinatarajia kurejea mazoezini leo baada ya mapumziko ya sikukuu ya Krisimasi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad