Yanga ya Moto Huku Simon Msuva, Kule Sankara Karamoko

Yanga ya Moto Huku Simon Msuva, Kule Sankara Karamoko

 

Yanga inaendelea na hesabu za usajili kimyakimya ikitaka kuboresha kikosi kabla ya kurejea katika michuano mapema mwakani ikiwamo Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu na kwa kuonyesha imepania, hivi unavyosoma kuna kigogo yupo njiani kwenda Ivory Coast kumaliza dili ya straika wa Asec Mimosas, Sankara Karamoko.


Akili za mabosi wa Yanga ni kutaka mchezaji huyo aungane fasta na Simon Msuva sambamba na nyota wengine waliopo kikosini ili kuleta balaa zaidi kwenye michuano inayoshiriki ikiwamo Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ikiwa na kiporo cha mechi za hatua ya 64 Bora dhidi ya Hausung ya Njombe.


Sankara ndiye mshambuliaji kiongozi wa mabao wa kikosi cha ASEC ya Ivory Coast, akiwa pia ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa na yupo kwenye hesabu kali za Yanga ili aje kwa msimu huu kuboresha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.


Yanga ilishafanya mazungumzo ya muda mrefu na Sankara na ikabakia hatua ndogo tu ya kwenda kumaliza dili hilo na unavyosoma habari hii kuna kigogo yuko njiani kwenda Ivory Coast kumalizia dili hilo.


Yanga ilibakiza hatua ndogo ya kukubaliana na klabu ya ASEC ambayo mshambuliaji huyo alibakiza mkataba mfupi wa miezi kadhaa ambapo wao walikuwa wanataka fedha ndefu kidogo wakiringia ofa moja ya klabu ya Denmark iliyokuwa inamtaka mshambuliaji huyo


Mwanaspoti linafahamu Yanga ndio wamemsuka Sankara kugomea dili hilo kutokana na klabu iliyokuwa inamtaka inacheza ligi ya chini zaidi na mshambuliaji huyo akajaa.


Yanga haitaki hadi fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zianze kabla ya kumalizana na nyota huyo ambaye pia wachezaji wenzake wa zamani Stephanie Aziz KI, Pacome Zouzoua na Yao Akouassi ndio wamesukuma wakimsisitiza Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said kumshusha jamaa huyo.


Hesabu za Yanga ziko hivi, inajua kuletwa kwa Sankara hataweza kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa tayari ameshasajiliwa ASEC, lakini mshambuliaji mzawa Simon Msuva atamaliza kiu hiyo, huku wataungana kwenye mechi za Ligi Kuu na ASFC, kwani yeye hajacheza michuano ya CAF.


Yanga inaona kama itamnasa Msuva basi ataisaidia Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa kisha wawili hao watakutana kwenye mashindano ya ndani.


Ujio wa nyota hao na kuungana na wachezaji wengine waliopo kikosini wataifanya Yanga itishe zaidi kwani langoni ataendelea kusimama, Diarra Djigui, huku kulia akiwa Yao Kouassi na kushoto Joyce Lomalisa, wakati mabeki wa kati wanatarajiwa kuendelea kutegemewa, Dickson Job na Ibrahim Bacca kama sio nahodha Bakar Mwamnyeto.


Eneo la kiungo kutakuwa na Khalid Aucho na Mudathir Yahya/Pacome Zouzoua, huku Sankara na Msuva watasimama eneo la ushambuliaji wakisaidiwa na Maxi Nzengeli na Stephane Aziz KI, wakati benchi litakuwa na nyota wengine ambao wamekuwa akitumiwa na Kocha Miguel Gamondi sasa atalazimika kukata wachezaji wawili wa kigeni akiwamo Hafiz Konkon na Gift Fred wameshindwa kufanya maajabu.


Ujio wa Msuva unaweza kula kichwa cha mtu kikosini akiwamo Crispin Ngushi, Denis Nkane ambao wameshindwa kumshawishi Gamondi kumtumia.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad