Aliyedaiwa kumuua mpenzi wake kwa kisu afariki dunia




Rombo. Mtuhumiwa anayedaiwa kusababisha kifo cha Beatrice Minja kwa kumchoma kisu mara 25, Lucas Tarimo, amefariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi wakati akiendelea na matibabu katika hospitali ya Huruma iliyopo Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Daktari kiongozi wa Hospitali ya Huruma wilayani hapa, Daria Mushi amethibitisha kifo hicho.

"Ni kweli Lucas Tarimo amefariki jana saa 4:30 usiku," amesema Dk Mushi.

Novemba 12, 2023 mwanaume huyo anadaiwa kumshambulia kwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wa mpenzi wake, Beatrice Minja (47) mkazi wa Kijiji cha Mbomai Juu, Tarakea ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC na Desemba 27,2023 alifariki dunia.

Hata hivyo, Desemba 31, 2023 Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, David Misime alieleza kuwa, Tarimo alikamatwa Desemba 31 alfajiri akiwa amejificha kijiji cha Jema, kata ya Oldonyosambu, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha akijiandaa kukimbilia nchi jirani.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kuona mkono wa Serikali unamfikia alikunywa sumu inayotumika kuua wadudu na alipatiwa huduma ya kwanza ili taratibu nyingine za kisheria ziendelee.

"Tunawashukuru sana wananchi wa kata hiyo kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Jeshi la Polisi hadi kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

“Ingawa baada ya kuona mkono wa Serikali unamfikia alikunywa sumu inayotumika kuua wadudu, mtuhumiwa amepatiwa huduma ya kwanza yupo vizuri na taratibu za kisheria zinaendelea," ilieleza taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi.

Awali mtoto wa marehemu Beatrice Minja, Glory Mchomba alilieleza Mwananchi kuwa wakati tukio hilo linatokea Novemba 12, 2023 mama yake huyo alikuwa anatokea kwenye kikundi na ndipo alipovamiwa na mwanaume huyo.

Anasema wakati akiwa nyumbani siku hiyo ya Jumapili, alipata taarifa kwamba mama yake yuko chini na hali yake sio nzuri na kumtaka aende kumchukua mama yake kumpeleka hospitali na ndipo alipokwenda na kumpeleka hospitali ya Huruma kabla ya kuhamishiwa KCMC.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad