Itakapotimu saa 2:15 usiku leo APR itakuwa Uwanja wa New Amaan Complex kupambana na Yanga lakini wanajeshi hao wa Rwanda wanaitaka sana mechi kulipa kisasi.
APR haijawahi kuifunga Yanga na mara ya mwisho timu hizo zilikutana Machi 12, 2016 ambapo Yanga ilitangulia kuwachapa wanajeshi hao kwa mabao 2-1 kwao jijini Kigali kwa mabao ya kiungo Thaban Kamusoko na Juma Abdul kwa njia ya adhabu.
Mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Mkapa Yanga ikasonga mbele ikilazimishwa sare ya bao 1-1 mchezo uliopigwa Machi 19, 2016 na hapo ndipo APR wanataka kuanzia.
Kipa wa APR Pavelh Ndzila amesema wanajua kwamba historia inawahukumu lakini wanataka kubadilisha hilo kwenye mchezo wa leo.
Ndzila amesema wanaiheshimu Yanga lakini wameisoma vizuri kwenye mechi tatu zilizopita na haitakuwa rahisi kwao kupoteza kutokana na ubora wa kikosi chao.
"Yanga ni timu nzuri sana lakini tutawashangaza tunataka kuanzia hapo kubadilisha hiyo historia, tunajua kwamba watakuja na kikosi tofauti na hata sisi tutakuja tofauti,"amesema Ndzila ambaye ni mmoja wa mastaa muhimu wa kikosi hicho.
"Tunataka kushinda hii mechi, tulipita hapa tunaona nafasi ya kuweka historia kwa kucheza Fainali, ili tucheze mechi hiyo tutapambana na hii klabu kubwa kwanza kwenye hatua hii,"