Asec Yatoa Masharti Ili… Sankara Karamoko Asaini Yanga





Mshambuliaji Sankara Karamoko
KLABU ya Asec Mimosas ya Ivory Coast imekubali kufanya mazungumzo rasmi na Yanga kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wake, Sankara Karamoko mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo mazungumzo hayo ya kumnunua mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 yatalenga zaidi usajili wa dirisha kubwa na sio hili dogo.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka Yanga kimeliambia Championi Ijumaa kuwa, Asec imeweka ngumu kumruhusu Karamoko kuondoka kwa sasa kutokana na kumhitaji kwenye michuano ya kimataifa.

Kiliongeza kuwa, hata hivyo Yanga  wamepewa ruhusa ya kufanya mazungumzo na Asec ya kuhusu usajili wa nyota huyo kupitia dirisha kubwa kwa faida ya timu pamoja na mchezaji mwenyewe.

“Wametuambia kuwa haiwezekani kwa sasa kufanyika biashara ya Karamoko Sankara kwa kuwa wanataka awasaidie katika michuano ya kimataifa ambapo kwa sasa wapo katika hatua nzuri ya kuweza kufuzu kwenda katika hatua inayofuata.

“Kingine kwa mchezaji ambaye kwa sasa anayeongoza kwenye mbio za ufungaji bora Ligi ya Mabingwa Afrika wanataka kumuona huenda akatimiza ndoto zake za kufanikiwa kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo hivyo wanataka kumpa nafasi zaidi tofuti na kumuuza.

“Kwahiyo wamesema mpaka dirisha kubwa la usajili ndio wanaweza wakafanya biashara lakini kwa sasa haiwezekani,” kilisema chanzo hiko.

Kwa upande wa Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa: “Sankara Karamoko tumemuona ni mshambuliaji mzuri kama ambavyo wamekuja kina Yao, Pacome na wachezaji wengine kutoka Asec basi hata Sankara anaweza akatua Yanga kwa kuwa Asec ni marafiki zetu na tunaweza kufanya nao biashara nzuri.”

Sankara Karamoko ni miongoni mwa washambuliaji ambao Yanga walikuwa wakiwahitaji kwa ajili ya kuwasajili dirisha hili dogo sambamba na Leonal Ateba wa Cameroon na Glody Kilangalanga.

Mshambuliaji huyo ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa nayo manne na asisti moja huku timu yake ya Asec ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.

Na Marco Mzumbe, Championi Ijumaa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad