Aziz KI apewa dk 87 Burkinabe ikichapa mtu Afcon 2023



KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI, amecheza kwa dakika 87 kwenye kikosi chake cha Burkina Faso wakati kikiichapa Mauritania bao 1-0 katika mchezo wao wa kwanza wa Kundi D wa fainali za Afcon 2020 huko Ivory Coast.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa La Paix, Aziz KI alianzishwa na kocha Hubert Velud katika mfumo wa 4-2-3-1 na kucheza kwa dakika 87, kabla ya kutolewa na kuingizwa Hassane Bande.

Wakati Mauritania wakidhani kwamba wataondoka uwanjani hapo na pointi moja, mambo yalitibuka baada ya kufanya madhambi ndani ya boksi kwenye dakika za majeruhi na kusababisha mkwaju wa penalti, uliowekwa nyavuni na winga matata, Bertrand Traore kuifanya Burkina Faso kuandikisha ushindi wao wa kwanza kwenye Afcon 2023 na kuongoza kundi lao, lenye timu za Algeria na Angola pia.

Burkina Faso na Mauritania zilishambuliana kwa zamu huku uimara wa kipa Herve Koffi uliisaidia timu hiyo ya staa Aziz KI kubaki mchezoni baada ya kuokoa hatari kadhaa.

Mchezo mwingine wa Kundi D uliofanyika usiku wa Jumatatu, uliwashuhudia Algeria na Angola zikitoshana nguvu baada ya sare ya bao 1-1. Algeria ya Riyad Mahrez ilitangulia kufunga kupitia kwa Baghdad Boundjah kwenye kipindi cha kwanza kabla ya Angola kusawazisha kipindi cha pili kwa mkwaju wa penalti ya Agustinho Mabululu.

ZOUZOUA, YAO WAMTAZAMA AZIZ KI
Wakati Aziz KI akifanya yake huko Ivory Coast kwenye mikikimikiki ya Afcon 2023, mastaa anaocheza nao Yanga, Pacome Zouzoua na Attohoula Yao walikuwa mbele ya televisheni zao kushuhudia kipute hicho na kurusha video kwenye mtandao wa Instagram wakionyesha namna wanavyomsapoti mwenzao kwa kutazama mechi.

Pacome na Yao wakiwa wametupia uzi wa klabu yao ya Yanga walirusha video ikionyesha migongo yao na televisheni ambayo ilikuwa inaonyesha mchezo huo wa Burkina Faso na Mauritania.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad