Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa kuanzia mwaka 2015, atafika mbele ya kikao hicho kesho Alhamisi Januari 25, 2024 kujibu tuhuma hizo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Joel Makwaiya alipotafutwa na Mwananchi Digital leo Jumatano, Januari 24, 2024 kujua undani wa kikao hicho amesema chama hicho kina utaratibu wa kujiendesha na katika hilo kesho Alhamisi kutakuwa vikao viwili, kikao cha usalama na maadili na kile cha siasa cha wilaya.
“Kikao cha usalama na maadili kinaweza kumuita mtu yoyote, lengo ni kukisaidia chama pale kinapohitaji kujua jambo lolote, ni mambo ya kawaida kuitana na kweli tumemwita akisaidie chama,” amesema Makwaiya.
Katika kusisitiza hilo, katibu huyo amesema, “yeye (Mpina) ni mwanachama wetu kama walivyokuwa wanachama wetu hapa Meatu, lakini pia ni mbunge wetu. Yapo mambo yaliyotokea tumemuita aje kutusaidia.” Waziri Bashe ampiga vijembe Mpina
Makwaiya alipoulizwa ni mambo gani hayo ambayo yametokea hadi aitwe na kamati ya usalama na maadili, hakuwa tayari kuyaeleza kwa kina, zaidi ya kusema, “ni mambo ya kawaida, tumemwita kama tunavyoweza kumuita mwanachama yeyote.”
Hata hivyo, Mpina hajapatikana katika namba zake za mkononi kwani ziliita bila kupokewa.
Ingawa Makwaiya hakuwa tayari kuweka wazi, lakini mmoja wa viongozi wa CCM wilayani humo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema Mpina ameitwa kutokana na kauli zake kuchonganisha Serikali, viongozi na wananchi.
“Unajua huyu ndugu yetu kama mnavyomfuatilia, amekuwa akipingana na Serikali, amekuwa akitoa kauli zinazochonganisha Serikali na wananchi na wakati mwingine unamwona anagombana na mawaziri bungeni,” amesema kiongozi huyo.
Amesema kitendo cha kuitwa katika kikao cha maadili, “lolote linaweza kumtokea, anaweza hata kupendekezwa kufukuzwa, kuonywa au chochote na unajua tunakwenda kwenye uchaguzi mwakani.”
Katika mikutano ya Bunge, Mpina amekuwa mwiba kwa mawaziri tangu alipowekwa kando kwenye Baraza la Mawaziri na karibu katika kila mkutano wa Bunge huibua mijadala mikubwa na kuwafanya mawaziri kunyanyuka kumjibu.
Mawaziri ambao mara kadhaa wamekuwa wakiguswa na michango yake ni wa fedha, miundombinu, ujenzi, nishati na kilimo. Miongoni mwao nii; Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Hussein Bashe (Kilimo), Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na January Makamba aliyekuwa Nishati sasa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mwananchi Digital limemtafuta Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Simiyu, Shamsa Mohamed kumuuliza kuhusu hilo lakini amesema hana taarifa za kikao hicho. Bato la mpina, Mwigulu bungeni
“Lakini vikao hivyo ni vya kawaida katika chama kuanzia ngazi ya tawi hadi mkoa na kama kuna hiyo kamati ya maadili ni vikao vya kawaida.”
Mwenyekiti huyo amesema katika chama hicho hakuna mtu aliye juu kwani ndicho kimewaweka madiwani, wabunge na viongozi wengine, kwa hiyo “hakuna aliyeko juu ya chama. Ukiona ameitwa ngazi ya wilaya hiyo ni ‘size’ yako, ukiona ameitwa hakuna mkubwa kwenye chama wala mkamilifu na ni vikao vya kawaida. Ukiitwa kule utakwenda kusikilizwa.”
Kanuni za uongozi na maadili za CCM zinaeleza mtu yoyote anayetuhumiwa mbele ya kamati ya usalama na maadili ya ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na maadili au nidhamu ya chama, atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma mbele ya wajumbe wa kamati hiyo.
Ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi lakini hataaambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama imekwisha kujulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya sheria au vyombo vya habari. Mpina alia na ufisadi
Kanuni hizo zinaeleza kamati ya usalama na maadili ya ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu suala hilo, kwenye kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa nakala ya uamuzi kwa maandishi.
Ikiwa mwanachama anayefikishwa mbele kamati ya usalama na maadili kutakuwa na adhabu mbalimbali zikiwemo za onyo na atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi sita.
Anayepewa onyo kali atakuwa chini ya uangalizi wa miezi 12. Adhabu ya karipio atawekwa chini ya matazamio ya miezi 18 na akiwa katika kipindi hicho, hatakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama lakini atakuwa na haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi wake wa chama.
Pia kuna adhabu ya kuvuliwa uanachama na au kuachishwa uongozi.