CCM Yamuweka Kikaangoni Mpina kwa Dk 120

CCM Yamuweka Kikaangoni Mpina kwa Dk 120


Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu ametumia saa mbili kumhoji Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina.


Waziri huyo wa zamani wa mifugo na uvuvi, amefika mbele ya kamati hiyo leo Alhamisi, Januari 25, 2024 katika ofisi za CCM wilayani humo kujibu tuhuma mbalimbali zinazomkabili ikiwemo kutofanya mikutano, kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.


Mpina aliyekuwa amevalia shati la kijani, suruali nyeusi na mkononi ameshika mkoba alifika katika ofisi hizo saa saba mchana na kupokelewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meatu, Antony Phillipo.


Baadaye aliingia katika kikao hicho kuanzia saa saba na kumalizika saa 9 alasiri. Kisha kikao kilibadilika kutoka kamati ya usalama na maadili na kuwa kikao cha siasa cha wilaya ambavyo vyote viliongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Abdillah Hajji.


Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, saa 10:05 jioni, Mwananchi Digital limemtafuta Mpina kutaka kujua kilichojiri, lakini hakuwa tayari kueleza kilichomfanya aitwe na kilichotokea.


“Sasa ndugu yangu si huyo aliyesema Mpina kaitwa basi yeye si ndio akwambie nini kimetokea?” amehoji Mpina.


Alipoulizwa nini kimeamuliwa kwenye kikao, Mpina amesema, “sina maoni yoyote katika hilo.”


Katibu wa CCM, Wilaya ya Meatu, Joel Makwaia aliyesema kikao kimefanyika na Mpina amehudhuria.


Alipoulizwa ni nini hasa alikuwa akituhumiwa na kilichofikiwa, Makwaia amejibu kwa kifupi, “mambo mengine ni ya ndani, wewe elewa tu kikao kimefanyika na Mpina alifika.”


Hatukuishia hapo, Mwananchi Digital limezungumza na Hajji aliyesema, “ni vikao vya kawaida tu kwa wanachama. Yeye (Mpina) ni mjumbe wa kamati ya siasa huwa anapaswa kuhudhuria na yeye huwa hahudhurii.”


Alipoulizwa sababu za kutokuhudhuria au mara ya mwisho alihudhuria lini, mwenyekiti huyo amesema, “yeye (Mpina) ana sababu nyingi za kutokuhudhuria.”


Mwananchi Digital ilipotaka kujua nini wameafikiana, amesema mambo ya vikao yanabaki katika vikao na si kuyaweka hadharani, “na isichukuliwe kwamba kuna tatizo kubwa ni mambo ya kawaida.”


Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho amesema wao kama chama waliona umuhimu wa kumuita Mpina mbele ya kamati ili awasaidie katika mambo yanayowaleta shida katika maeneo yao.


“Kubwa zaidi lililotufanya sisi kama wajumbe wa hii kamati ni kujua kwa nini haonekani jimboni, hafanyi mikutano ya wananchi, hasikilizi kero za wananchi na kazi yake kulumbana na wenzake huko na kukifanya chama kififie huku,” amesema mjumbe huyo aliyeomba hifadhi ya jina.


“Sasa alikuja, kaja na wapambe wanne ambao hawakuruhusiwa kuingia mkutanoni na kwa kweli ana majibu ya kawaida sana, anasema anafanya mikutano, sasa tunamuuliza mikutano amefanya wapi na wapi na lini, majibu hatujayaelewa kwa kweli,” amesema.


Mjumbe huyo amesema, “mwaka huu ni uchaguzi wa Serikali za mitaa, mwakani uchaguzi mkuu, sasa mtu wa kuchangamsha ni mbunge, kama hafanyi mikutano, hasikilizi kero na kuzitafutia ufumbuzi nani atafanya hivyo?”


Katika kusisitiza hilo, mjumbe huyo amesema, “unajua hili jimbo (la Kisesa) lina asili ya upinzani, kwani limewahi kuongozwa na upinzani mara mbili mwaka 1995 na 2000, sasa watu wanataka kumwona mbunge na yeye haonekani na jimbo linapaswa kuwa karibu na mwenye jukumu hilo ni mbunge ambaye ndiye huyu ambaye haonekani.”


Alipoulizwa nini wamekubaliana baada ya kuwa wamemhoji, amesema, “hilo sasa kwa kweli tuliache ni la kwetu, lakini nafikiri viongozi wetu watapeleka uamuzi wetu ngazi ya juu ambao ni mkoa na Taifa. Huu uamuzi wetu ndio utaamua waukubali au waukatae au vinginevyo.”


Katika mikutano ya Bunge, Mpina amekuwa mwiba kwa mawaziri bungeni, miongoni mwa waliokumbana na maswali yake na hoja zinazoibua mijadala ni Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Hussein Bashe (Kilimo), Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na January Makamba aliyekuwa Nishati (sasa yupo Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).


Adhabu zinazoweza kumpata


Kanuni za uongozi na maadili za CCM zinaeleza mtu yoyote anayetuhumiwa mbele ya kamati ya usalama na maadili ya ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na maadili au nidhamu ya chama, atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma mbele ya wajumbe wa kamati hiyo.


Ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi, lakini hataaambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama imekwishajulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya sheria au vyombo vya habari.


Kanuni hizo zinaeleza kamati ya usalama na maadili ya ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu suala hilo, kwenye kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa nakala ya uamuzi kwa maandishi.


Ikiwa mwanachama anayefikishwa mbele kamati ya usalama na maadili kutakuwa na adhabu mbalimbali zikiwemo za onyo na atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi sita.


Anayepewa onyo kali atakuwa chini ya uangalizi wa miezi 12. Adhabu ya karipio atawekwa chini ya matazamio ya miezi 18 na akiwa katika kipindi hicho, hatakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama, lakini atakuwa na haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi wake wa chama.


Pia kuna adhabu ya kuvuliwa uanachama na au kuachishwa uongozi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad