DC Msando ajibu kuhusu kudaiwa Sh175 milioni

 
DC Msando ajibu kuhusu kudaiwa Sh175 milioni

Mahakama Kuu imewaamuru wafanyabiashara Albert Msando na Jacquelene Msando, kumlipa mfanyabiashara Bahati Mgonja anayemiliki kampuni ya Y&H Mgonja Enterprises, Sh175 milioni kama fidia ya biashara ya vinywaji.

Hii ni baada ya mrufani wa kwanza, The Don’s Group Tanzania ya jijini Arusha na Albert Msando na mkewe Jacquelene kushindwa rufaa waliyoifungua Mahakama Kuu, kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Albert Msando, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, yeye na mkewe ndio wamiliki wa klabu maarufu ya The Don’s Lounge ya jijini Arusha inayofanya vizuri kibiashara katika jiji hilo la utalii.

Hata hivyo, Msando amesema atakata rufaa hukumu ya Mahakama Kuu, akisema mawakili wake wako katika mchakato wa kupinga hukumu hiyo, akitoa sababu mbili.

“Tutakata rufaa kwa hukumu hiyo. Hoja yangu ya kwanza ni kwamba biashara inayolalamikiwa ni kati ya Y&H Mgonja Enterprises na The Don’s Group Tanzania, mimi ni mwanahisa na mkurugenzi, kwa hiyo biashara sijafanya mimi, bali The Don,” alisema.

Alitaja sababu ya pili kuwa ni mmoja wa ndugu wa Bahati Mgonja (Innocent Mgonja), ambaye ndiye alikuwa akiwaletea vinywaji na alichukua fedha hizo na kuandika jina kwenye daftari, lakini mdai (Bahati Mgonja) anamkana.

“Tunakata rufaa Mahakama ya Rufani, tayari mawakili wangu wameshaipata hukumu, tutapinga uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisema.

Kesi ilivyokuwa

Bahati Mgonja anayefanya biashara kwa jina la Y&H Mgonja Enterprises, alifungua kesi ya madai Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, akidai malimbikizo ya madai ya Sh181.2 milioni zilizotokana na deni la vinywaji alivyowauzia wadaiwa hao.

Mbele ya mahakama, wadaiwa hao walikanusha madai hayo na kueleza kuwa walimlipa mfanyabiashara huyo kwa kutumia utaratibu wa hundi au fedha taslimu kwa mtu waliyemtaja kuwa ni Innocent Mgonja baada tu ya kupokea bidhaa.

Hata hivyo, mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimpa ushindi mfanyabiashara huyo na kuwaamuru wadaiwa hao watatu, kulipa Sh155 milioni kama madai halisi ya biashara na Sh20 milioni kama malipo ya fidia ya jumla ya biashara hiyo.

Albert Msando ambaye ni mwanashria kitaaluma pamoja na wadaiwa wenzake, hawakuridhishwa na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha wakiegemea katika hoja nane kupinga hukumu hiyo.

Miongoni mwa sababu hizo ni kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kuhitimisha kuwa kulikuwa na makubaliano baina ya warufani hao na mjibu maombi na pia kuhitimisha kuwa kulikuwa na bidhaa walizopewa bila uthibitisho.

Pia walieleza kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kuhitimisha katika hukumu yake kuwa The Don’s Group Tanzania na wenzake walikiri deni hilo kupitia utetezi wao wa maandishi katika kesi hiyo katika aya ya 6 na 7 kuwa ni kweli wanadaiwa.

Halikadhalika walieleza kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kuegemea ushahidi wa nyaraka ambao haukutolewa mahakamani kama kielelezo, na kwamba hakimu huyo alikosea pia kisheria pale alipowaamuru kulipa jumla ya Sh175 milioni.

Mabishano ya kisheria kortini

Novemba 7, 2023 rufaa yao ilipoitwa mbele ya Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, wakili wa warufani, Allen Godian na mjibu rufaa ambaye ni Bahati Mgonja, waliomba kuwasilisha hoja za kesi hiyo kwa njia ya mawasilisho.

Katika hoja zao, wakili wa kina Msando, Allen Godian alieleza hapakuwepo makubaliano kati ya pande hizo mbili ambayo yaliidhinishwa na mjibu maombi anayefanya biashara kwa jina la Mgonja Enterprises, yawe ya kimaandishi au ushahidi wa mdomo. Kulingana na wakili Godian, kwa kuwa kiwango kilichodaiwa na Mgonja kilizidi Sh200 milioni, basi makubaliano hayo yalipaswa yathibitishwe na mkataba kwa vile warufani walikuwa wanakana kuingia makubaliano wala kukiri kudaiwa.

Wakili huyo aliieleza mahakama kuwa kulikuwa hakuna ushahidi wowote unaojenga msingi kuwa Albert Msando na Jacquelene Msando waliingia makubaliano hayo, hasa ikizingatiwa hawafanyi biashara kwa kutumia majina yao.

Kwa upande wake, mjibu rufaa hiyo, alieleza kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha unaohusiana na makubaliano ya uuzaji wa vinywaji mbalimbali kwa pande hizo mbili na kwamba warufani hao walikiri uwepo wa makubaliano hayo.

Alisema kwa kuwa Albert Msando na Jacquelene Msando ni wanahisa na wakurugenzi wa mrufani wa kwanza, The Don’s Group Tanzania, basi kushtakiwa kwao kulikuwa ni sahihi kisheria na kwamba wanafungwa na utetezi wao.

Alichokisema Jaji kwenye hukumu

Katika hukumu yake aliyoitoa Januari 24, 2024 na nakala ya hukumu hiyo kupatikana katika mtandao wa mahakama hiyo hiyo Januari 24, Jaji Gwae alichambua hoja za pande zote mbili na kutupilia mbali rufaa ya kina Msando.

Jaji Gwae alisema wajibu aliokuwa nao ulikuwa ni kupitia kumbukumbu za mahakama za kesi hiyo kuthibitisha kama ni kweli warufani kwa njia moja ama nyingine, walikiri uwepo wa makubaliano ya mauziano ya vinywaji hivyo.

Kwa mujibu wa Jaji, majibu yao ya pamoja ya maandishi ya utetezi ya Albert na Jacquelene yaliyowasilishwa mahakamani, yako wazi kuwa walibishania juu ya kuwepo makubaliano ya kuuziwa vinywaji mbalimbali na mjibu maombi.

Hata hivyo, Jaji alisema warufani hao walikubali uwepo wa mahusiano kati ya mrufani wa kwanza ambaye ni The Don’s Group Tanzania, lakini wakakanusha kudaiwa na kueleza kuwa malipo ya mauziano yalilipwa kwa mjibu maombi.

“Kwa hicho nilichokinukuu sehemu ya 2 na 3 ya wasilisho lao mahakamani, ni kama kusema kulikuwa na makubaliano ya mauziano ya vinywaji kati ya The Don’s Group Tanzania na mjibu rufaa hiyo (Mgonja),” alisema.

Aliongeza: “Ukisoma utetezi wa mrufani huyo wa kwanza katika aya ya 4, 6, 7, 8, 9, 10 na 11 unaona kuna maudhui ambayo ni kukiri kwa kuwepo uhusiano uuzianaji wa vinywaji kati ya mjibu maombi (Mgonja) na The Don’s Group Tanzania.”

“Kuhusiana na lalamiko kuwa mrufani wa pili (Albert) na wa tatu (Jacquelene) hawakustahili kushtakiwa wao kama watu binafsi, naona hoja hii inakosa mashiko, hasa ikizingatiwa kuwa wao ni wanahisa na wakurugenzi wa The Don’s Group.”

Kutokana na sababu hizo na nyingine ambazo Jaji alizizingatia, alisema rufaa hiyo haikufanikiwa na kwamba uamuzi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha unathibitishwa na kuwaamuru Msando na wenzake kuli
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad