KUTOKA Mbagala hadi kumfunga Liverpool katika pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya sidhani kama tunamheshimu Mbwana Samatta kama inavyostahili. Kutoka Mbagala hadi kuifunga Manchester City katika pambano la fainali ya Carabao kwenye Uwanja wa Wembley, uliopo London, England sidhani kama tunampa Samatta heshima anayostahili.
Mambo mawili. Nilikuwa natazama mechi za Afcon nikiwa na Watanzania wenzangu. Lawama ni nyingi kwa Samatta. Kitu cha kwanza kabisa naweza kushuhudia miguu mizito ya Samatta kwa sasa. Umri unamchukua.
Zamani Samatta angeweza kuchukua mpira upande wa kushoto akaanza kuwalamba chenga mabeki wa timu pinzani kuanzia upande wa kibendera cha kushoto hadi kibendera cha kulia. Sasa hivi naona kasi hiyo imetoka. Inatokea kwa kila mchezaji. Hata kwa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo inawatokea sasa hivi.
Sasa hivi anajaribu kucheza mpira rahisi. Amebakiwa na kasi ndogo mguuni, lakini bado inatusaidia. Kama ambavyo alifanya wakati alipopika bao la Simon Msuva katika pambano dhidi ya Zambia.
Wakati akiwa katika ubora wake tulimlaumu Samatta. Na sasa akiwa hayupo katika ubora wake bado tunamlaumu Samatta. Kisa? Akiwa katika katika ubora wake Samatta alijikuta katika timu ya taifa ambayo amezungukwa na rundo la wachezaji wa kawaida.
Akiwa na Gent na timu nyingine alizopitia Samatta alikuwa mmaliziaji zaidi. Angeweza kusimama mbele na kusubiri mipira. Katika timu yetu Samatta muda mwingi anarudi nyuma kuchota mipira na kuipeleka mbele. Muda mwingi anageuka katika kiungo mchezeshaji. Unadhani anapenda? Hapana. Anachezea timu ambayo haimtengenezei nafasi. Analazimika kuchukua majukumu mengine.
Majukumu haya yamekausha mabao yake kwa muda mrefu. Mtu ambaye ananufaika ni Msuva. Na Msuva anapofunga huwa tunasema. “Msuva anajituma sana katika timu ya taifa kuliko Samatta.” Kisa? Samatta hajafunga mara kwa mara.
Wakati huu tukiendelea kumkejeli Samatta bado tunabakia wanafiki tu. Hatutaki kuona ukweli kwamba Samatta anapocheza nusu tu ya uwezo wake kama ilivyo sasa, basi wachezaji wetu wengi wa eneo lake hawafikii uwezo wake.
Hata hii Afcon ameonyesha kitu hicho. Pamoja na ‘uzee’ wake, lakini bado anaweza kuutunza mpira mguuni akaogopwa na wapinzani. Hapa pia tuna unafiki fulani hivi. Wakati Adel Amrouche alipomtoa nje Samatta katika pambano la Zambia kuna watu wengi walisikika wakidai. “Samatta alipotoka Zambia wakapunguza hofu wakaanza kuja mbele.”
Hawa ndio Watanzania. Upande wa moyo unamkejeli Samatta, upande mwingine unamkubali. Katika nchi nyingine Samatta angeishia benchi kwa sababu kungekuwa na mastaa wengi waliochomoza na kuwika Ulaya ambao wangestahili nafasi mbele yake. lakini tuonyesheni mastaa hao katika soka la Tanzania. Wako wapi?
Wachezaji wanastahili kukosolewa lakini binafsi huwa nakaa kimya linapokuja suala la Samatta. Ana makosa yake ya kibinadamu kabisa uwanjani. Hata hivyo, yanapaswa kukoselewa kwa heshima. Samatta ndiye ambaye amesababisha watoto wetu waote ndoto na kuziamini.
Anastahili kukosolewa kwa heshima kubwa. Samatta ndiye alama yetu. Kabla yake tuliamini kwamba Mtanzania hawezi kutamba Ulaya. Hawezi kufunga bao Wembley katika pambano la fainali za wazungu. Hawezi kuwa mfungaji bora Ligi Kuu ya Ubelgiji. Hawezi kucheza Ligi ya Mabingwa na kuifunga timu kama Liverpool.
Alichofanya ni kutuachia alama. Amesababisha watoto wetu waamini. Zamani tulidhani Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo angekuwa kama hawa wa dizaini hii ya kina Haji Mnoga ambao wamezaliwa Ulaya na kukulia huko.
Hata hivyo, yeye alijiamulia mwenyewe safari yake kutoka Mbagala na kufika alikofika. Hakuna watu wengi wanaoweza kujisifu kwamba walipambania ndoto yake. kwani kuna wachezaji wangapi wanaosimamiwa na wanaishia kutuaibisha?
Aliamua mwenyewe kuipambania ndoto yake na sasa anakuwa mhanga wa ndoto zake mwenyewe. Amekuwa mkubwa zaidi kiasi kwamba sasa amegeuzwa kuwa jalala. Bahati mbaya hii anayo pia mtu kama Mohamed Salah.
Bahati mbaya, hii pia angeweza kuwa nayo Sadio Mane. Uzuri wa Mane ni kwamba ana watu wa kumfanyia kazi katika kikosi cha timu ya taifa. Wapo kina Kalidou Koulibaly, Edo Mendy, Idrisa Gana Gueye, Ismail Sarr na wengineo. Wanamsaidia kazi. Vinginevyo Mane angeweza kuishia kuwa kama Samatta tu.
Binafsi ningekuwa Samatta ningestaafu katika kikosi cha timu ya taifa. Sijui mwenyewe anafikiria nini kwa sasa. Nadhani imetosha. Lawama zisizo na msingi ambazo anapewa nadhani ingekuwa mimi ningesema inatosha. Watanzania hatuna jema.
Tunaweza kumsulubu kwa kinachotokea dakika tisini lakini tungekuwa na heshima kidogo basi tungekumbuka namna gani alivyokuwa mwema katika soka letu. Soka letu lilihitaji alama na ameiweka. Ni kama alama ambayo Diamond Platinumz ameiweka katika muziki.
Hajawahi kutokea mchezaji kama Samatta katika taifa letu lakini bado watu wanamchukulia kuwa mchezaji wa kawaida tu kama wengine. Lakini hapo hapo tunaweza kujiuliza, anapata kitu gani cha msingi anapoamua kusafiri maili nyingi kurudi nyumbani kuichezea timu ya taifa? Unaamini kwamba Taifa Stars inamlipa zaidi ya klabu zake anazochezea barani Ulaya?
Ni uzalendo tu ndio ambao unamfanya aendelee kuipigania Taifa Stars lakini mara nyingi anachoambua ni lawama zilizopitiliza. Sidhani kama tunamuheshimu sana kama ambavyo wenzetu wanafanya kwa mastaa wao wakubwa.
Diego Maradona alikumbwa na kashfa ya kutumia dawa zisizoruhusiwa michezoni wakati alipoenda katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 pale Marekani. Hata hivyo, Waargentina walisimama nyuma yake kwa sababu wanajua kwamba ni alama ya taifa lao katika soka. Na wakati huo mpira ulikuwa umeondoka mguuni kwake.
Sisi anajitokeza shabiki mmoja asiye na mbele wala nyuma na kumtupia Samatta matusi ya nguoni kwa sababu tu ameshindwa kutuliza mpira vema au amepiga shuti lililokwenda nje. Wenzetu wana akili timamu linapokuja suala la kuheshimu mtu aliyeacha alama. Mtu ambaye amesababisha tuanze kuwaruhusu watoto wetu kucheza soka tukiamini wanaweza kufika Ligi Kuu ya England.
Binafsi niliamini kwamba siku moja ingefika na Samatta angeweza kuwa kama hivi alivyo. Kwani uliamini kwamba siku moja Messi angekuwa hana soko Ulaya na angecheza Marekani? Lakini pindi mambo yanapofika hivi kwa wenzetu heshima bado inaendelea kuwa juu na hawatoi lugha za kashfa kwa mashujaa wao.
CREDIT:- MWANASPOTI