Familia ya mwanafunzi Mtanzania aliyeuawa Israel yaanua msiba





Arusha. Familia ya mwanafunzi Joshua Mollel, aliyetekwa na kuuawa kwenye mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza imeanua msiba, huku wakiendelea kusubiri mwili au mabaki ya mwili wa kijana wao.

Mbali na Joshua, mwingine waliotekwa pamoja ni Clemence Mtenga (22) ambaye mwili wake ulirejeshwa  nchini mwaka jana na kuzikwa nyumbani kwao, Kijiji cha Kirwa Mashati, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro. 

Mtenga alikuwa ni muhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA) ambao walikwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo, chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na nchi hiyo.

Leo Jumatano, Januari 10, 2024, akizungumza na Mwananchi Digital kujua nini kinaendelea juu ya Joshua, msemaji wa familia hiyo, Ephata Nanyaro amesema waliweka msiba kwa muda wa siku 14 kuanzia Desemba 17 hadi 31, 2023, baada ya kuona video iliyowahakikishia kuwa Joshua ameuawa.

“Msiba tulianua bila kufanya kitu chochote ila tuna matumaini kuwa mwili utapatikana, Serikali ya Israel iliahidi familia kuwa itajitahidi kupata mwili au mabaki hivyo kwa sasa tunasubiria kutoka huko Israel.

“Msiba tuliuweka kuanzia Desemba 17, 2023 baada ya kuona ile video mtandaoni ambayo ilituhakikishia Joshua ameuawa na tulianua Desemba 31, 2023 kwa taratibu za Kikristo kwani sisi ni familia inayoamini kwenye dini hiyo," amesema.

Joshua alitekwa na wanajeshi hao Oktoba 7, 2023 ambapo baada ya video iliyokuwa ikionyesha alivyokamatwa na wanajeshi hao kusambaa mitandaoni, simanzi ilitawala katika familia ya baba yake, Loitu Mollel, mkazi wa eneo la Orkesmet wilayani Simanjiro,Manyara.


Desemba 29, 2023,Mollel aliwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), akitokea Israel alikofia mwanaye na kuwaambia  waandishi wa habari uwanjani hapo kuwa alisafiri Desemba 24, 2023 kwenda nchini humo kwa ajili ya wito wa Serikali ya Israel.

Alisema “Kwa kifupi ilikuwa safari ya huzuni, safari isiyokuwa na matumaini, tulichozungumza na Serikali ya Israel wamenieleza hali halisi jinsi ilivyokuwa wale maharamia walivyoingia na kuanza kuua watu bila huruma.

Mzazi huyo amesema alifika hadi sehemu aliyokuwa anaishi kijana wake na kukutana na mwanafunzi mwenzake ambaye alimweleza jinsi siku hiyo ilivyokuwa.

 Kuhusu kijana wake kudaiwa kuwa mwanajeshi, Mollel alikanusha madai hayo na kueleza alimlea kijana wake mwenyewe na hakuwa mwanajeshi wala mgambo.

“Nimemlea mimi kule alikwenda yuko shamba, hajawahi kuwa hata mgambo ila sasa wale wanaosema alikuwa mwanajeshi au alikuwa mgambo siwaambii lolote mimi, lakini Mungu yupo, kwa sababu wakati mwingine watu wanazusha habari ambazo hawazifahamu hata kidogo,”alisema.

Joshua alikuwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne wa Mzee Mollel, alikwenda Israel Septemba mwaka jana kwa lengo la kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa muda wa miezi 11.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad