RAIS Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kutangazwa mshindi kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika hivi karibuni. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi Congo (CENI), Denis Kadima, Rais mteule Tshisekedi, ameshinda baada ya kupata asilimia 73 za kura zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo leo Jumapili, Kadima amesema aliyekuwa mpinzani wa karibu na Tshisekedi, Moise Katumbi, amepata asilimia 18, wakati aliyeshika nafasi ya tatu, Martin Fayulu akiambulia asilimia Tano.
Felix Tshisekedi, Rais wa DR Congo
Kabla matokeo hayo kutangazwa, wapinzani pamoja na baadhi ya waangalizi wa uchaguzi waliukosoa kwa madai kuwa haukuwa huru kutokana na kughubikwa na dosari kadhaa, ikiwemo baadhi ya vifaa kuharibika na vituo vya kupigia kura kuchelewa kufunguliwa.
Sheria ya uchaguzi ya DRC inaruhusu watu kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi, lakini Katumbi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema hawezi kuchukua hatua hiyo kwa madai kuwa mahakama za Congo haziko huru.
Katumbi ambaye ni mfanyabiashara maarufu nchini humo, harakati zake kuwania urais zilikuwa ngumu baada ya kudaiwa hana asili ya Congo Kwa kuwa mama yake alikuwa Mzambia na baba yake Myahudi.
Kufuatia matokeo hayo, Rais Mteule Tshisekedi ataapishwa kushika muhula wa pili wa urais wa Congo tarehe 20 Januari 2024.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini Congo, wanasema ushindi wa Rais mteule Tshisekedi unatokana na kuungwa mkono na raia waishio maeneo ya vijijini ambao wamezielewa sera zake za kupambana na vikundi vya waasi nchini humo ili kurejesha amani.