Serikali imekiri kufahamu suala la kutopata ajira kwa vijana waliokuwa wakijitolea kwa muda wa miaka miwili katika Manispaa ya Iringa, lakini ajira zilipotoka hawakupata kutokana na kutofuatwa kwa taratibu wakati wa usaili.
Kauli hiyo iimetolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum mkoani Iringa, Ritha Kabati.
“Mheshimiwa Spika kwa mijibu wa taarifa tulizopewa pale vijana walionekana kuwa wamefeli katika mitihani lakini kiukweli kulionekana kwamba kuna figisu zimefanyika katika kuhakikisha kwamba wamefikia hayo matokeo na ndipo Serikali ilipoelekeza kuwa mchakato huo uangaliwe tena upya. Ndio maana ninapozungumza hapa hakuna majibu ya wale ambao wamekwishaajiriwa kwa sababu zipo taratibu zinafanyika.” Amesema Naibu Waziri Kikwete.
Katika swali lake Mbunge Ritha Kabati alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa kwa baadhi ya viongozi wasiotekeleza matamko yanayotolewa na Viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo Mawaziri.