Angola ilimaliza kinara wa Kundi D ikiwa na alama saba [7] baada ya kupata ushindi dhidi ya Mauritania na Burkina Faso na kutoka sare dhidi ya Algeria.
Kwa upande wa Namibia, iliandika rekodi kwa kushinda mchezo wake wa kwanza na pekee kwenye michuano ya AFCON ushindi ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kufuzu kwenye hatua ya mtoano.
Stade de la Paix sio uwanja mgeni kwa Angola, wametumia uwanja huo kwa michezo yao miwili ya hatua ya makundi.
Nyota wa Namibia, Deon Hotto amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Brave Warriors akiwa ameshinda tuzo ya Man of the Match mara mbili kwenye hatua ya makundi.
Kwa upande wa Angola, Gelson Dala ambaye ametajwa kwenye kikosi bora cha CAF cha hatua ya makundi, amefunga magoli mawili kwenye hatua ya makundi anaweza kuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Namibia.
Makocha wa timu zote mbili wanafuraha baada ya timu zao kufanikiwa kufuzu hatua ya mtoano. Bado wanamatumaini timu zao zinaweza kufanya vizuri kwenye hatua ya 16 bora na kuandika historia zaidi kwenye mashindano.
Pedro Goncalves-Kocha Mkuu, Angola.
“Imekuwa historia ya aina yake kwetu, tuna mchezo mkubwa na muhimu mbele yetu. Inawezekana ni mchezo mkubwa zaidi kwa timu ya Angola kwa miaka 14 iliyopita.”
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda mbele ya Namibia. Utakuwa mchezo mgumu lakini ninaimani kila mmoja wetu atatelekeza majukumu yake.”
Collin Benjamin-Kocha Mkuu, Namibia.
“Tuna wachezaji wazuri kiufundi na wenye uwezo mkubwa, kuna wachezaji ambao walikuwa sehemu ya timu tangu 2019 kwa hiyo kuna mwendelezo.”
“Tuna timu nzuri na wachezaji wanafuraha na wanahitaji kufanikiwa zaidi, tunafahamu nini cha kufanya, ni muhimu kuwa imara sana kwenye eneo letu la ulinzi.”
“Tunataka kuwa sehemu ya timu bora 16 za Afrika na hatimaye tumekuwa miongoni mwa timu bora 16, ni jambo linalotupa hamasa.”