Hii Hapa Simba Mpya ya Kocha Benchikha



USAJILI uliofanywa na Simba katika dirisha dogo la usajili pamoja na mashindano ya Kombe la Mapinduzi unaweza kubadili hali ya mambo katika kikosi hicho wakati mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika yatakaporejea.

Jana mchana timu hiyo ilifanya usajili wa kushtukiza wa mshambuliaji wa Gambia, Pa Omar Jobe kutoka FC Zhenis ya Kazakhstan ambaye amechukua nafasi ya Moses Phiri aliyetupiwa virago.

Hadi jana mchana, Simba ilikuwa imewasajili, Pa Omar Jobe, Ladack Chasambi, Boubacar Sarr, Saleh Masoud ‘Karabaka’ na Edwin Baluwa ambao wanapishwa na Jimmyson Mwanuke, Shaban Chilunda, Nassoro Kapama na Feruzi Teru ambao wanaenda kutafuta changamoto mpya kwingineko.

Usajili huo unafanya kusababisha mabadiliko kadhaa katika kikosi cha Simba ambapo wapo wachezaji wanaweza kuwa na uhakika wa nafasi katika kikosi cha kwanza, wengine wanaonekana kuwa katika uwezekano mkubwa wa kuwa mpango mbadala wa benchi la ufundi la Simba chini ya Abdelhak Benchikha lakini kuna ambao nafasi zao zinaweza kuwekwa rehani ama iwe katika kikosi cha kwanza au benchi.

PA OMAR JOBE NI NANI?

Huyu ni mshambuliaji ambaye anaonekana hana uzoefu na soka la Afrika akiwa ametumika muda mwingi nje ya bara hili, timu iliyompa mafanikio zaidi ni Sheikh Jamal ya Banglandesh ambayo aliitumikia kwenye michezo 88 na kufunga mabao 10.

Kuanzia hapo, ametumika kwenye timu nne, Zhenis, Neman Grodno, Shkendija na Struga akiwa amefunga mabao matano tu kwenye timu zote, lakini akiwa amecheza mechi mbili za timu ya Taifa ya Gambia

HAWA MAMBO SAFI

Mambo yanaonekana kuwa mazuri kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa hatarini kupigwa panga na Simba kabla ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi lakini baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye mashindano hayo, hapana shaka wamefanikiwa kushinda imani ya kocha Benchikha ambaye anaweza kuwapa nafasi kubwa ya kucheza pindi mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam na Ligi ya Mabingwa Afrika zikirejea.


Hussein Kazi aliyekuwa chaguo la nne katika nafasi ya beki wa kati, sasa anaelekea kuwa chaguo la tatu nyuma ya Che Fondoh Malone na Henock Inonga ambao ndiyo wamekuwa mabeki wa kati wanaoanza kikosini.

Winga Luis Miquissone, ana nafasi kubwa ya kurejea kwenye kikosi cha kwanza tofauti na ilivyokuwa katika mechi za mwanzoni mwa msimu kutokana na unyumbulifu wa hali ya juu aliouonyesha, uwezo wa kupiga chenga na kasi, vitu ambavyo mwanzoni mwa msimu huu hakuweza kuvionyesha kwa kuathirika zaidi na kile kinachoonekana kutokuwa fiti ingawa sasa ameonyesha kurudi vizuri.

Mchezaji mwingine ni kipa Hussein Abel ambaye alidaka vyema katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na APR ambao ulipomalizika alitangazwa kuwa mchezaji bora na hapana shaka ndiye amechangia kuachwa kwa kipa kinda wa Simba, Ally Feruzi.

MASTAA 8 UHAKIKA

Wachezaji wanane wanaonekana kutokuwa na hofu ya kupoteza nafasi katika mechi zilizosalia za msimu huu kutokana na imani ambayo kocha Abdelhak Benchika anaonyesha kuiweka kwao isipokuwa kama watashindwa kutunza viwango ndio wanaweza kujikuta wakimtibua kocha huyo.

Nyota hao wameonekana kupata nafasi ya mara kwa mara ya kucheza chini ya Benchikha na hapana shaka licha ya timu hiyo kufanya usajili katika dirisha dogo, wataendelea kuwa kipaumbele kwa kocha huyo.

Kuna wanne wanaocheza katika safu ya ulinzi ambao ni mabeki Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Inonga na Che Malone.

Kiungo aliye kwenye kiwango bora hivi sasa, Fabrice Ngoma ana nafasi kubwa ya kuendelea kupata nafasi ya kucheza kikosini na kwa vile Boubacar Sarr ni pendekezo la Benchikha, kiungo huyo Msenegal ana nafasi kubwa ya kuingia katika kikosi cha kwanza na hivyo kibarua kinabaki kwa Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin ambao hapana shaka watapaswa kupambana vilivyo ili waweze kucheza mbele ya Ngoma na Sarr.

Ugumu unaonekana kuwa mkubwa zaidi kwa Abdallah Hamisi ambaye kabla hata ya ujio wa Sarr, hakuwa akipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba.


Wachezaji wengine wawili ambao Benchikha anaonekana kuwakubali zaidi kikosini ni Willy Onana na Saido Ntibazonkiza ambao chini yake wamekuwa wakianza kikosi cha kwanza mara kwa mara.

KIKOSI CHA KIBABE

Kwa usajili ambao Simba imefanya katika dirisha dogo pamoja na kiwango kilichoonekana kwenye Kombe la Mapinduzi kwa baadhi ya wachezaji, kocha Benchikha sasa angalau anaweza kushusha pumzi kutokana na kuwa na wachezaji wanaompa kikosi cha kwanza chenye ushindani lakini ameongezewa idadi ya kutosha ya wachezaji katika benchi ambao wanaweza kumpa mpango mbadala katika mechi tofauti.

Benchikha anaweza kuanza na kikosi chenye kipa Aishi Manula na safu ya ulinzi itakayoundwa na Malone, Mohammed Hussein, Inonga na Kapombe huku viungo wawili wa chini wakiwa ni Fabrice Ngoma na Sarr.

Viungo watatu wa juu katika mfumo wa 4-2-3-1 wanaweza kuwa Willy Onana, Ntibazonkiza na Kibu Denis wakati mshambuliaji wa kati atasimama Jobe.

Katika benchi, Benchika anaweza kumpanga yeyote kati ya Ayoub Lakred, Abel au Ally Salim kama mbadala wa Manula huku akiwa na Israel Mwenda na David Kameta kama wasaidizi wa mabeki wa pembeni na Hussein Kazi kama mbadala wa beki ya kati.

Wasaidizi wa Ngoma na Sarr ni Mzamiru na Kanoute na upande wa viungo/mawinga wa juu kuna Chasambi, Miquissone na Karabaka.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad