Mwimbaji wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Diamond Platnumz amekuwa akifungua biashara na kuwekeza katika miradi mbalimbali kwa kile anachoita kuigopa kesho yake pale hatapokuwa hafanyi tena muziki.
Hajawahi kuweka wazi utajiri wake ni kiasi gani lakini tunaweza kupata picha mara baada ya kuikata ripoti iliyodai utajiri wake ni Dola5.1 milioni, wastani wa Sh12.8 bilioni kwa kueleza utajiri wake ni zaidi hapo.
Katika kuhakikisha kesho yake haikumbwi na njaa kali kama mwenyewe alivyodai, Diamond amefanikiwa kutengeneza sura tatu katika biashara zake hadi sasa kama ifuatavyo;
1. Biashara zilizopo sasa Ukiachana na muziki wake, hizi ni biashara tano ambazo Diamond ameziweka wazi kwa mashabiki wake ambazo zinamuingizia fedha kwa wakati huu.
A. WCB Wasafi Huu ndio uwekezaji wa mwanzo kabisa wa Diamond tangu alipoanza muziki, alianzisha lebo hii baada ya kuachana na Sharobaro Records. Mwaka 2015 alianza kusaini wasanii akianza na Harmonize, kisha Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice.
Kupitia lebo hii wasanii anaowasimamia wamefanya vizuri, mfano; Rayvanny ndiye msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo ya BET, huku Harmonize na Zuchu wakishinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama wasanii Bora Chipukizi pindi alipowatoa.
B. Wasafi Media Mwaka 2018 alitambulika kama msanii wa kwanza Tanzania kumiliki vyombo vya habari (electronic media) baada ya kuanzisha Wasafi Radio na TV, anatajwa kuwa msanii wa pili barani Afrika kufanya hivyo baada ya Youssou N'Dour wa Senegal.
Hata hivyo, mkongwe wa Bongofleva, Joseph Mbilinyi 'Sugu' ambaye alikuwa Mbunge kwa miaka 10 anatajwa kama msanii kwanza kumiliki chombo cha habari (print media) ambapo mwaka 2002 alianzia gazeti lake, Deiwaka.
C. Zoom Extra Hii ni kampuni ya kutengeneza video za muziki ambayo awali ilijulikana kama Zoom Production, mabadiliko hayo ya jina inadaiwa ni baada ya Harmonize kuondoka WCB Wasafi na ndio mwanzilishi wa Zoom Production.
Zoom Extra ambayo imefanya video nyingi za wasanii wa WCB Wasafi, ilitikiswa mara baada ya Director Kenny aliyoanza nayo tangu mwanzo kuondoka na kwenda kuanzisha kampuni yake, DK Limited. Tangu kuondoka kwa Kenny, Zoom Extra haijaonekana kuwa na nguvu ile ya mwanzo.
2. Biashara zilizosimama Hizi ni biashara nyingine za mwanzo za Diamond baada ya WCB Wasafi Lebo, hizi ziliingia sokoni lakini hazikuweza kuwa na wakati mzuri na kusimama hadi wakati huu.
A. Wasafi.com Mtandao wa Wasafi.com ulianzisha kwa lengo la kuuza na kusambaza muziki wa wasanii, Diamond alikuwa msanii wa kwanza Tanzania kufanya hivyo lakini duniani kuna wasanii wengi waliofanya hivyo kama Jay Z na mtandao wa Tidal ingawa aliununua kwa Dola56 milioni mwaka 2015.
Hata hivyo, mtandao huo uliingia sokoni wakati tayari mitandao mengi kutoka nje imekita mizizi ya kibiashara hiyo kwa muda, na sasa Wasafi.com haipo tena hewani, huku mitandao yake kijamii tangu Oktoba 2018 ikiwa haijatoa taarifa zozote.
B. Chibu Perfume Hii ilitengenezwa Dubai na bei yake ikiwa ni zaidi ya Sh100,000, licha ya promosheni kubwa mradi huo haukuweza kulishika soko kwa kipindi kirefu na hatimaye Chibu Perfume ikaondoka kabisa sokoni.
Ikumbukwe baada ya Diamond, msanii mwingine wa Bongofleva, Mwana FA ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naye alikuja na bidhaa zake za manukato, Fyn By Falsafa.
C. Diamond Karanga Baada ya kuonekana Chibu Perfume ilikuwa biashara iliyolenga zaidi tabaka la juu ambalo limefanikiwa kichumi, Diamond alisema atakuja na bidhaa ambazo zitawagusa kabisa watu wake wa chini.
Bidhaa hizo ni Diamond Karanga ambazo bei yake ilikuwa ni Sh300 tu kwa pakiti moja, hii lifanya vizuri sana na kupendwa na watu wengi lakini ghafla bidha hizo zilipotea sokoni.
3. Biashara zinazongojewa Kila Mfanyabiashara anakuwa na mipango ya mbeleni kuhakikisha anakuza au kulinda kipato chake, ndivyo ilivyo kwa Diamond, hii ni miradi yake mingine ambayo ipo mbioni.
A. Wasafi Tower Jengo hili Diamond alieleza kuwa lipo maeneo ya Mikocheni Dar es Salaam na litakuwa na Ofisi na Hoteli, pia lebo ya WCB Wasafi na biashara zake nyingine zitahamia hapo.
Kufika Oktoba 2021 Diamond alitumia ukurasa wake wa X (Twitter) kutaarifu umma kuwa ujenzi wa Wasafi Tower umefikia asilimia 95, hivyo muda wowote watu wataona jengo hilo, hadi sasa mashabiki wake wanasubiria.
B. Air Wasafi Julai 2022 Diamond akiongea na DW Africa alithibitisha kununua ndege kwa lengo la kile alichoita ni kuongeza thamani yake, na baadaye alikuja kuweka wazi mipango yake kuanzisha shirika la ndege, Air Wasafi.
Hata hivyo, muda ambao ndege hiyo ilitarajiwa kuwasili Tanzania haikuwasili hadi leo, Diamond alisema suala hilo lipo kwenye vyombo vya sheria kufuatia mtu aliyepewa jukumu hilo kutotimiza makubaliano yao.
C. The Real Life of Wasafi Hapo Juni 19, 2018 Diamond alitangaza kuanza kwa kipindi cha televisheni kitakachokuwa kinaonyesha maisha ya watu wote wanaohusikana na WCB Wasafi na bidhaa zake.
Hii ni biashara nyingine ya Diamond inayongojewa kwa hamu kubwa na mashabiki wake kwani na yeye atakuwa sehemu ya kipindi hicho. Ikumbukwe baadhi ya Mastaa Bongo wamewahi kuwa na TV Show zao, miongoni mwao ni Fid Q, Lady Jaydee, Chidi Benzi na Wema Sepetu.