IGP Wambura Afunguka: Polisi Hafi Kizembe
Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura amesema pamoja na kwamba askari wa jeshi hilo wanatakiwa kutumia nguvu ya kadiri wanapopambana na wahalifu, hawatakiwi kufa kizembe.
Amesema hayo leo Januari 4, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, baada ya mkutano wa makamanda wa polisi wa mikoa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni.
Kauli ya IGP Wambura imekuja kufuatia tukio la kuuawa kwa vijana wawili Bakari Ismail (21) na Shomari Kacheuka maarufu Babuu (22) wakazi wa Vingunguti Jijini Dar es Salaam, huku Jeshi la Polisi likithibitisha kuwapiga risasi zilizosababisha vifo vyao na wengine walikimbia.
"Panyarodi ni vijana wenye umri wa kati na mdogo ambao hutumia silaha za jadi hususani mapanga, visu, nondo kujipatia vipato vya uhalifu na hujeruhi watu na mara nyingi wamesababisha vifo kwa wananchi ambao wamekuwa wakipora mali zao,” amesema Wambura.
Amesema polisi kama binadamu wengine, hawapaswi kufa kizembe.
“Polisi ni binadamu kama walivyo binadamu wengine, lakini polisi hulazimika kufa kwa sababu za msingi anapokuwa anatetea haki, maisha na mali za raia wa nchi hii. Hatakiwi kufa kizembe,” amesema.
Kuhusu polisi kutumia nguvu akiwa na silaha aliyokabidhiwa, amesema anatakiwa kutumia nguvu ya kadiri.
“Nguvu anayotumia askari kwenye ground ndiye anayetafsiri nguvu hiyo, kuanzia kumkamata shati, mkono na nguvu hiyo huenda hadi kuua kulingana na nguvu ya panyarodi,” amesema.
Akiendelea kujibu maswali ya waandishi wa habari, IGP Wambura amezungumzia tukio la mwanamke anayetambulika kwa jina la Beatrice Minja aliyefariki dunia baada ya kuchomwa kisu mara 25 na mpenzi wake aliyetajwa kwa jina Lucas Tarimo (marehemu) wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.
Licha ya tukio hilo kutokea Novemba 12, 2023 tukio lilifichuliwa mitandaoni Desemba 26 na Desemba 27 mwanamke huyo alifariki katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
IGP Wambura amesema ilikuwa bahati tu mtuhumiwa alipatikana baada ya mwanamke huyo kufariki dunia Desemba 27, 2023.
“Ukamataji ni process, ni kwamba ilitokea kama coincidence (bahati) kwamba baada ya taarifa siku tatu akakamatwa, si kwamba ni mtandao (uliofichua),” amesema.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayehusika katika tukio la uhalifu.
Amesema Serikali inafuatilia malalamiko hayo na itamchukulia hatua mtu yeyote atakayehusishwa na tukio la uhalifu.
"Nataka niwahakikishie vilevile, tukio lolote la kihalifu ambalo limefanywa na mtu yoyote, yakiwamo hayo matukio ambayo yamejtokeza ya aina yoyote, hakuna hata tukio moja ambapo hakuna hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa.
“Iwe tukio limefanywa na raia, au limefanywa na mtu yeyote,” amesema huku akiwataka wananchi wawe na imani na Jeshi la Polisi.
mwananchi.co.tz