Simba inaendelea na mazoezi kambini Mo Simba Arena, jijini Dar es Salaam chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, huku kukiwa na taarifa za kushtua juu ya kocha huyo kutoka Algeria ambayo hivi karibuni imeaga fainali za Kombe la Afrika (Afcon) 2023.
Ipo hivi. Shirikisho la Soka Algeria linapiga hesabu ndefu za kumsaka mtu wa kurithi nafasi ya kocha mkuu wa mabingwa wao wa Afrika wa 1990 na 2019 baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Djamel Belmadi kupoteza ajira baada ya kuishia makundi katika fainali za Afcon kule Ivory Coast, huku Benchikha akitajwa.
Inaelezwa kati ya makocha watatu wanaopigiwa hesabu na shirikisho hilo, yumo Benchikha ambaye ni raia wa nchi hiyo na wengine wawili wenye asili ya taifa hilo.
Makocha wengine wanaotajwa sambamba na kocha huyo wa Simba ni; Jean Fernandez aliyezaliwa mji mmoja maarufu wa French Algeria ambao ulitumika kumaliza ukoloni wa Ufanransa kwa taifa hilo, pia yumo Rabah Madjer.
Mapema jaribio wa Algeria hao kumchukua Zineddine Zidane ambaye ana asili ya taifa hilo, liligonga mwamba baada ya kocha huyo wa zamani wa Real Madrid kugomea ofa hiyo. Zidane ni raia wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria akiwa na mafanikio makubwa ya kubeba Kombe la Dunia 1998 enzi akiwa mchezaji.
Zizzou pia ametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa Super Cup, Klabu Bingwa ya Dunia mbali na La Liga na Kombe la Ligi akiwa Real Madrid, kwa sasa hana timu na Algeria ilimpigia hesabu lakini akachomoa ndio maana wakaamua kuwanyemelea Benchikha na wenzake.
ACHOMOA
Licha ya Algeria kuonyesha nia ya kumtaka Benchikha inadaiwa amegoma kuiweka kichwani ofa hiyo na kutaka kuelekeza akili yake Simba.
Benchikha, aliyeanza kazi juzi ya kuendelea kukinoa kikosi hicho, aliliambia Mwanaspoti akili yake sasa ipo kwenye kusaka mafanikio zaidi akiwa Simba na hana mawazo ya kurudi kwao.
“Nadhani bado ni mapema sana kufikiria kuondoka hapa (Simba), kuna safari ambayo tumeianza kati yangu na klabu hii siku chache zilizopita haitakuwa sawasawa kuondoka kwa haraka, nadhani atapatikana kocha mzuri baada ya rafiki yangu Djamel,” alisema Benchikha aliyefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na USM Alger ya Algeria na kuongeza;
“Kuna mambo nataka kuyakamilisha hapa Simba ili iwe klabu yenye mafanikio zaidi Afrika na hata hapa Tanzania, nafurahi kuona wachezaji nao wanataka haya mafanikio kwahiyo tumeanza kazi hivi sasa.”
NYUMBA UFUKWENI
Akiwa na Simba Benchikha amefanya kwa vitendo akiwapa mtihani mkubwa mabosi wake akitaka kutafutiwa nyumba ya kuishi eneo la Masaki.
Benchikha hataki kukaa hotelini, katika masharti aliyowapa mabosi wake anataka nyumba ambayo akitoka nje tu mlangoni atakutana na upepo mzuri wa bahari ya hindi.
Simba katika msako huo wa nyumba italazimika kutumia kiasi cha dola 2000 sawa na Sh 5 milioni kwa mwezi.