JUZI kati hapa, Simba ilimshusha Mzimbabwe Michael Charamba aliyetarajiwa kuchukua mikoba ya Clatous Chota Chama ndani ya kikosi cha timu hiyo, lakini hajaonekana kumudu kuvaa viatu vya Mzambia huyo. Baadaye ikamtambulisha kiungo wa chini, Msenegal, Babacar Sarr, ambaye aliwahi kumkaba Cristiano Ronaldo kule Saudi Arabia.
Wakati mashabiki wakitarajia kuona mchezaji mwingine wa kigeni akishushwa, tayari kengele ya hatari imeshalia, timu hiyo inatakiwa kukata mchezaji mmoja ili Sarr aingie kwenye kikosi na kutimiza idadi ya wachezaji 12 wa kigeni wanaoruhusiwa kikanuni.
Hapo pia hatma ya Mzimbabwe ikiwa shakani.
Wakati hali ikiwa hivyo, watani wao wa jadi, Yanga nao wameshikwa pabaya na sheria hiyo ya wageni 12, wanatakiwa kuwakata wachezaji wawili ili Augustine Okrah na straika Pame Glody Kilangalanga kutoka katika klabu ya Bisha FC ya Saudi Arabia, waweze kuingia kwenye usajili.
Gamondi anataka winga anayeweza kuingia ndani na anayeweza kuzalisha mabao mengi.
Kuna wachezaji ambao wako kwenye wakati mgumu ndani ya klabu hiyo ambao ni Hafiz Konkoni, Jesus Moloko na Mahlatse Makudubela 'Skudu'.
Konkoni anaonekana kuwa ni chaguo jepesi zaidi kutemwa kwa kuwa hajafanya kile ambacho straika huyo alikuwa akitarajiwa kukifanya akiwa amefunga bao moja tu kwenye Ligi Kuu Bara na hapati nafasi ya kucheza na taarifa za ndani zinasema straika huyo wa Ghana anataka kubaki Jangwani, lakini kama klabu hiyo italazimisha kumweka kando, hayuko tayari kutolewa kwa mkopo, anaona ni heri avunjiwe mkataba apewe maokoto yake.
Skudu amekuwa akizua mitazamo tofauti. Baadhi wanaona ana msaada kwa timu na hata zile mbwembwe zake za uwanjani zinatosha kuwapa raha mashabiki akitimiza cheo chake cha mtaani cha 'Waziri wa Raha'; lakini wahafidhina wanaona mchezaji wa kigeni ambaye inatarajiwa atakuwa analipwa pesa nyingi kuliko wazawa, hapaswi kuwa haaminiwi kuchezeshwa katika mechi za ushindani mkubwa na badala yake kuingizwa uwanjani katika dakika chache za mwisho za mechi ngumu ambayo 'ishamalizwa' na wenzake au kuishia kuchezeshwa katika mechi dhidi ya timu za daraja la kati kama Mtibwa au KMC tu.
GIFT FRED KAPINDUA MEZA
Viongozi wanataka Moloko abaki Yanga kutokana na nidhamu yake anayoionyesha ndani ya timu hiyo, lakini kocha anaelezwa kuwa anataka mchezaji huyo akatwe kwa vile hampi kile anachokitaka uwanjani.
Nafasi yake kwa kiasi kikubwa inaweza kurithiwa na Okrah, ambaye kwa kawaida huwa ni tishio zaidi anapolielekea lango la wapinzani kwa kujua kufunga au kusaidia wenzake kufunga.
Beki wa kati, Gift Fred, awali alikuwa miongoni mwa ambao wangetemwa kirahisi zaidi Yanga, lakini sasa ameonekana kupindua meza baada ya kuonyesha uwezo mzuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambako Wananchi waling'olelewa katika hatua ya robo fainali baada ya kulala 3-1 mikononi mwa APR ya Rwanda.
Kocha Gamondi ambaye mwanzo hakuwa anamwelewa beki huyo, amemeza mate ya akili na kufikiria iwapo mmoja kati ya mabeki wake watatu -- Bakari Nondo Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job -- akikosekana kwa majeraha ama kutumikia adhabu ya kadi, Mganda huyo anaweza kuziba nafasi hiyo vizuri huku Yanga ikikabiliwa na mashindano mengi kuanzia Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika hadi Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
SIMBA INAMKATA NANI?
Bado hatma za Chama na Mzambia mwenzake, Moses Phiri hazijulikani ndani ya timu hiyo. Sakata la Chama bado limekwama kule kwenye Kamati ya Maadili. Phiri hana furaha ndani ya timu na aliomba kuondoka Msimbazi, mkataba wake unafikia tamati mwishoni mwa msimu.
KWANINI PHIRI?
Viongozi wanaweza kufikia mwafaka wa kuachana na Phiri kwa sababu sio kipenzi cha viongozi. Inadaiwa katika mkataba wake kulikuwa na kipengele cha kuongezewa pesa kadiri atakavyokuwa akifunga mabao.
Kipengele hicho inasemekana ndicho kilichosababisha mmoja kati ya viongozi wa Simba kumwambia kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' asiwe anamtumia mshambuliaji huyo.
Ni baada ya Phiri kupona majeraha akiwa ameshatupia mabao 10 msimu uliopita. Phiri hakupata nafasi na kuwafanya mashabiki na wanachama wa Simba kuhoji kulikoni.
Hata, alipokuja kocha Abdelhak Benchika, Phiri amekuwa hapati nafasi kubwa ya kutumika hususani kwenye mechi za kimataifa tofauti na ilivyotarajiwa na wengi.
Ikumbukwe Phiri alikuja Simba akiwa ametoka kutikisa nyavu mara 16 kwenye Ligi ya Zambia na kama angekuwa akipewa nafasi angeweza kupachika mabao mengi zaidi.
Viongozi wa Simba wanaweza kukubaliana na mchezaji huyo aondoke kabla ya mkataba wake haujaisha lakini hawataki abaki Dar es Salaam, wanaamini Yanga wanaweza kumchukua.
Salama ya Phiri kubaki Msimbazi ni kama Simba italiondoa jina la winga Aubin Kramo kwenye usajili wa sasa ili staa huyo wa Ivory Coast aendelee kujiuguza kisha aje kurejeshwa kikosini katika usajili wa dirisha kubwa.
WASIKIE MAKOCHA
Aliyekuwa kocha wa Yanga, Kenny Mwaisabula 'Mzazi' alisema engekuwa amepewa jukumu la kupunguza watu, angeondoa jina la straika Hafiz Wontah Konkoni (23) aliyesajiliwa kabla ya kuanza kwa msimu huu kutoka Bechem United ya kwao Ghana.
"Tofauti na wenzake kina Jesus Moloko na Mahlatse Makudubela 'Skudu' kuna wakati wanashitua watu, ila Konkoni hajaonyesha, kuhusu Simba sijui kwa nini sijaifuatilia, hivyo siwezi kuzungumzia lolote," alisema.
Kocha Meja Mstaafu Jeshi, Abdul Mingange alisema: "Ni ngumu sana kusema nani akatwe kwenye hizo timu, kwa sababu zina makocha wao na kila kocha ana mifumo yake na bado zinaendelea kusajili.
"Mfano Yanga imemsajili Augustine Okrah ana faida mbili, anaweza akacheza namba 10 na pembeni, sasa labda Gamondi anataka Aziz Ki akichoka Okrah amsaidie, kwa Simba ujio wa Babacar Sarr labda kocha anataka Fabrice Ngoma apande kucheza juu na Sarr chini, sasa nani akatwe nawaachia makocha wao".