Hatimaye Kamati ya waamuzi ya Zanzibar imemaliza utata ikisema mwamuzi wa mchezo wa Singida Fountain Gate Nasri Salum 'Msomali' hakuwa sahihi kuwapa shambulizi la kona wekundu hao.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Waziri Shekha amesema baada ya kikao kilichofanyika leo Januari 11, 2024 kupitia ufanisi uliofanywa na Msomali na wasaidizi wake wamegundua kwamba mwamuzi huyo hakuwa sahihi kwenye uamuzi wake huo wa kuwapa kona Simba.
Shekha amesema kosa hilo ni la kibinadamu kwani waamuzi nao hufanya makosa ambapo wamebaini ndio kosa pekee alilofanya Msomali ni kwenye mchezo huo wa jana usiku.
Msomali alitoa kona kwa Simba dakika ya 90 +8 ambayo ililalamikiwa na Singida, shambulizi ambalo liliwapa nafasi Simba kusawazisha bao hilo wakati ikiwa nyuma kwa bao 1-0 na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
"Nilikwambia kwamba tutachunguza na tumekutana leo kikao ambacho kimemalizika dakika chache zilizopita tumebaini kwamba kulikuwa na makosa kwa mwamuzi," amesema Shekha ambaye ni mwamuzi mstaafu.
"Haikupaswa kuwa kona hakuna sehemu ambayo mpira uliochezwa na mchezaji wa Singida na kipa aliudakia nje hivyo haikuwa sahihi kuwa kona, haya ni makosa ya Kibinadamu na ndio kosa pekee ambalo tumeliona baada ya kupitia ripoti na marudio sehemu zingine zote alikuwa sahihi.
"Tumeona hakuna sababu ya kumpa adhabu kubwa zaidi ya kumuonya kwasasa, kwanza mashindano haya yamebakiza mechi moja ya fainali lakini narudia hili ni kosa moja kati ya mazuri aliyoyafanya kwenye mchezo husika, tumemuonya na kumtaka awe makini asirudie makosa ya namna hii."
Aidha Shekha amejibu madai ya kwamba mwamuzi huyo kuchezesha mechi mbili za Singida dhidi ya Simba kwenye mashindano hayo.
Msomali alitangulia kuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi ya makundi baina ya timu hizo kisha ule wa Jana usiku, Singida wakiona haikuwa sahihi.
"Nikweli amechezesha mechi hizo lakini huyu ni mwamuzi mkubwa hapa mwenye beji ya FIFA na huu ulikuwa mchezo mkubwa unaozihusisha timu kubwa na zenye wachezaji wa Kimataifa kwahiyo hakukuwa na mbadala zaidi yake kuchezesha mechi hiyo."