Kapama afunguka baada ya kutemwa Simba



SIKU moja baada ya kupewa mkono wa kwaheri na timu ya Simba, mchezaji kiraka Nassor Kapama amesema huu ni wakati sahihi kwake kuondoka kwenda kujaribu changamoto nyingine nje ya timu hiyo.

Mchezaji huyo ambaye ameitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja na miezi sita, ameiomba klabu hiyo kumvunjia mkataba ili akajaribu maisha mengine nje ya Simba.

Awali, Simba ilifikia makubaliano ya kutaka kumtoa mchezaji huyo kwa mkopo kwenda Mtibwa Sugar lakini akagoma na kuomba avunjiwe mkataba ili aweze kwenda timu anayoitaka akiwa huru.

"Ni kweli nimepewa barua na Simba ya kunitoa kwa mkopo kwenda Mtibwa Sugar, ila nimeuomba uongozi tumalizane ili nichague timu ninayotaka kwenda," amesema mchezaji huyo.

"Kuhusu kuondoka Simba ilikuwa ni suala la muda kwani nilikuwa sipati nafasi ya kucheza, hivyo nilihitaji kuondoka ili kwenda kutafuta timu ambayo itanipa nafasi ya kucheza."

Kapama anasema hadi sasa upande wake ana ofa kutoka timu sita ambazo ni Ihefu FC, Geita Gold, Mashujaa FC, Mtibwa Sugar, JKT Tanzania na Namungo FC.

"Ofa ni nyingi nimepokea ikiwemo Mtibwa Sugar ambao walitaka kunichukua kwa mkopo kutoka Simba. Hadi sasa bado sijafanya uamuzi wapi naenda ila kabla ya dirisha kufungwa nitasajili timu ambayo itanipa ofa nzuri," anasema.


Tangu alipotua Simba, Kapama amecheza zaidi ya mechi 10 za mashindano ilizocheza timu hiyo ikiwemo Kariakoo Derby timu hiyo iliposhinda mabao 2-0 msimu uliopita.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad