Kenya wakubali yaishe, waondoa vikwazo ATCL




Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeondoa zuio walilokuwa wameweka kwa Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kufanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Nairobi kuanzia Januari 22, 2024.

Uamuzi huo umefikiwa baada Mamlaka ya Usimamizi wa Anga Kenya kukubali ombi la Tanzania la kutumia viwanja vyake kwa ajili ya safari za ndege za mizigo la Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwa vyombo vya habari na TCAA, kupitia Mkurugenzi wake, Hamza Johari.

“Mamlaka ya Usimamizi wa Anga Kenya imebariki kwa mujibu wa kifungu namba tano safari zote za ndege za mizigo kufanyika kama ilivyokuwa imeombwa na Serikali ya Tanzania kuanzia Januari 16, 2024,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na suala hilo, TCAA imeondoa zuio lililokuwa limewekwa awali kwa ndege za KQ kufanya safari zake kati ya Nairobi na Dar es Salaam.

KQ imekuwa ikifanya safari 33 kwa wiki kati ya Nairobi na Dar es Salaam ambayo ni sawa na wastani wa safari nne kwa siku.

Kupitia safari hizo kwa mujibu wa tovuti ya KQ, baadhi ya aina za ndege zilizokuwa zikitumika katika safari hizo ni Boeing 787.8, Boeing 737-700, Boeing 737-800, Boeing 737-300 na Embraer – E190 zenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 140.


Awali, alipozungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema Tanzania iliomba kufanya safari zake za ndege ya mizigo mara mbili kwa wiki kwenda Dubai kupitia Nairobi na kurudi.

Kabla ya uamuzi huo kutangazwa, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya waliingilia kati suala hilo baada ya wasiwasi kuibuka miongoni mwa wasafiri wa miji hiyo mikubwa Afrika Mashariki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, January Makamba na mwenzake wa Kenya, Musalia Mudavadi kupitia mtandao wa kijamii wa X waliweka bayana kufanya mazungumzo yaliyozaa azimio la kumaliza tofauti hizo ndani ya siku tatu.

Wawili hao walisema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa wamezielekeza mamlaka za usafiri wa anga katika mataifa hayo kufanya kazi pamoja na kuhakikisha wanamaliza jambo hilo.

Hata hivyo, KQ pia iliwatoa hofu wasafiri wake juu ya kile kilichofanyika, ikisema, “KQ inawasiliana na mamlaka za usafiri wa anga, taasisi za Serikali za Kenya na Tanzania zinazohusika ili kupata suluhisho linalotoa uhakika wa kutokatishwa kwa safari kati ya Nairobi na Dar es Salaam,” inaeleza taarifa kwa umma ya KQ iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano.

Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Donath Olomi aliliambia Mwananchi kuwa, vitendo kama hivyo na matamko yake yanaweza kukimbiza wawekezaji.

“Matamko kama haya yanafanya eneo letu lisionekane kuwa zuri kibiashara, sehemu zenye vita za aina hii zinaweza kukimbiza wawekezaji na wakaangalia sehemu gani nyingine wanayoweza kuitumia kwa ajili ya shughuli zake,” alisema Dk Olomi.

Alisema ni vyema vitu kama hivyo vikawa vinajadiliwa na kumalizika chinichini kabla ya kufika kwa jamii.

Dk Tobias Swai wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema ni vyema jambo kama hili linapotokea, faida za kiuchumi ziangaliwe zaidi kwa kuwa uwepo wake unarudisha nyuma maendeleo ya ukanda wa Afrika ya Mashariki (EA).

“Afrika ya Mashariki ni muungano, vitu kama hivi vinarudisha nyuma maendeleo yake. Ni vyema bodi za usuluhishi zitumike zaidi ndani ya ukanda huu kutatuta matatizo kama haya,” alisema Dk Swai.

Katika taarifa iliyotolewa Januari 15 na TCAA inaeleza kuwa, uamuzi uliokuwa umefanywa awali na Kenya ulikuwa kinyume na mkataba wa mashirikiano.

“Uamuzi uliofanyika ni kinyume cha kifungu namba nne cha mkataba wa ushirikiano wa huduma za anga kati ya Kenya na Tanzania ulioingiwa Novemba 24, 2016.” Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuheshimu mkataba wa Chicago wa mwaka 1944 na makubaliano ya ushirikiano katika anga kati yake na mataifa mengine.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad