Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimemsimamisha Mwenyekiti wa Chama hicho mkoani Dodoma, Yohana Mussa kwa madai ya kutoa kauli kinzani na msimamo wa chama hicho kuhusu miswaada mitatu ya sheria za uchaguzi.
Miswada hiyo ni ile inayohusu Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa iliyowasilishwa bungeni, Novemba 10 2023.
Mussa alikuwa miongoni mwa viongozi wa vyama kadhaa vya siasa waaliozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kupinga maandamano ya Chadema yaliyopangwa kufanyika Januari 24.
Vyama hivyo ni ACT Wazalendo iliyowakilishwa na Mussa, CUF, NCCR Mageuzi, AAFP, ADC na Demokrasia Makini.
Siku moja ya tamko la vyama hivyo, ACT Wazalendo imetoa taarifa leo Januari 19, 2024 ikieleza kumsimamisha Mussa.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari Uhusiano na Umma wa chama hicho, Janeth Rithe, imesema “Ndugu Yohana Mussa ambaye alitoa kauli kwa vyombo vya habari zinazokinzana na msimamo wa chama chetu kwenye miswada hiyo mitatu amesimamishwa uongozi na kutakiwa kujieleza.”
“Suala lake litapelekwa kwenye kikao kijacho cha Kamati Kuu kwa ajili ya maamuzi,” imeongeza taarifa hiyo bila kugusia suala la maandamano ya Chadema.
Taarifa hiyo imesema Kamati Kuu ya ACT Wazalendo kitakutana Januari 27, 2024 kwenye kikao chake cha kawaida, ambapo pamoja na mambo mengine itafanya tathmini juu ya hali ya kisiasa nchini ikiwemo kuangazia mwenendo wa mambo ndani na nje ya Bunge kuhusu mjadala wa miswada hiyo.
Ameandika kuwa ACT Wazalendo ipo macho kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mambo katika mjadala wa kitaifa unaoendelea kuhusu Miswada ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
“Chama chetu kilitoa rai kwa Serikali na Bunge kuhakikisha miswada hiyo inafanyiwa maboresho makubwa hasa kwa kujumuisha masuala ambayo tayari yalipata muafaka wa kitaifa na kukubalika na wadau wengi.
“Jopo la viongozi wa chama chetu likiongozwa na Kiongozi wa Chama Zitto Kabwe liliwasilisha maoni yake mbele ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. Ni imani yetu maoni hayo ambayo kwa hakika ndio maoni ya wadau wengi, yatazingatiwa.”
Mwananchi