Kocha Benchikha Alivyoibadili Timu ya Simba

 

Kocha Benchikha Alivyoibadili Timu ya Simba

Simba inaendelea kupita ukanda wa mabadiliko ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha tangu aanze kazi Novemba 29, 2023 akichukua nafasi ya Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.


Kuna mambo matano ambayo yamejionyesha kwa haraka, ndani ya Simba kuna mtu mpya amepitisha faili lake ambalo linajidhihirisha kupitia mabadiliko ya nje ya uwanja na hata ndani ya uwanja.


NIDHAMU KWANZA


Hili ni eneo kubwa ambalo Benchikha ameanza nalo, Simba ilikuwa na shida kubwa ya nidhamu kikosini, shida kubwa ya kikosi chake ilikuwa hapa. Robertinho aliangukia hapa hayo mengine yalikuwa ni ziada sana.


Ndani ya wachezaji wa Simba kulikuwa na matabaka mawili, yaani kundi la wachezaji wasioelezwa lolote wao ni wakubwa kuliko hata viongozi na hakuna mtu mwingine kwenye benchi la ufundi ilikuwa hata ukitaka kumbadilisha anamjia juu huyo mtu anayefanya hivyo.


Benchikha ameliondoa hili haraka, sasa wachezaji wa Simba wote wapo levo sawa hakuna anayejiona mkubwa kuliko wengine amepitisha sheria ambazo sio tu anataka azione zinafuatwa na ameanza kuzitumia.


Mfano ni jinsi alivyoanza na kiungo Clatous Chama, nani angeweza kumgusa Chama hapo kabla? Itakumbukwa Robertinho aliwahi kuambiwa yeye ndiye anayetakiwa kuingia kwenye mfumo wa kiungo huyo Mzambia na sio mchezaji kutii anachotaka kocha.


Chama hayupo Simba na hakuna anayemuulizia sasa, ingawa haivunji ukweli kwamba Chama ni mchezaji mzuri, Benchikha amesimamia nidhamu ameanza na mchezaji mkubwa baada ya hapo haitakuwa kazi kumbadilisha Israel Mwenza au Salehe Masoud ‘Karabaka’ wote atawaonoza kirahisi kwa kanuni zake.


ISHU YA MUDA


Hapo kabla ndani ya Simba ilikuwa rahisi kusikia mchezaji fulani hajakwenda kwenye ratiba ya kifungua kinywa yaani chai ya asubuhi lakini Benchikha amefuta hilo kila mmoja anatakiwa kuwa mezani kwa muda uliopangwa bila kuchelewa hata dakika moja ukichelewa yatakukuta na kibaya zaidi wala hataki kuambiwa yeye mwenyewe utamkuta mezani ‘amevimba pale’.


Eneo lingine lililokuwa la mazoea kwa wachezaji wa Simba ni kuchelewa kuanza safari za mazoezini au hata kwenye mechi, hilo limeshaondoka unavyosoma makala haya, muda wa kuondoka ukifika hakuna ambaye anabaki wala kuchelewesha msafara hata kwa nusu dakika itakula kwako.


HATAKI MCHEZO MAZOEZINI


Akiwa mazoezini Benchikha hataki masikhara ni kazi kazi, lakini pia anataka kuona umakini  sio mtu wa kumbembeleza mchezaji kivile kama ambavyo ilikuwa inafanyika nyuma vikao vingi, anachofanya anaelekeza au wasaidizi wake watakueleza kinachotakiwa kufanyika na baada ya hapo wanataka kuona unabadilika na sio kuendelea kufanya makosa yaleyale.


Ni rahisi kwa Benchikha kumuona anageuka mbogo hata kutamani kurusha chupa ya maji pale anapoona mchezaji wake anafanya makosa hatarishi au kurudia makosa yaleyale, kifupi anataka akili kubwa itawale uwanjani muda wote.


ANATAKA KUJIAMINI


Kuna tukio lilijionyesha hapa Unguja wakati kipa wa Simba Ally Salim akimsukuma beki wake Che Malone Fondoh Sasa yale ndio mambo anayoyataka Benchikha huko nje wala msiumize vichwa na kumuona kama kipa huyo alikosea.


Benchikha anawataka wachezaji wake kukosoana ikibidi hata hatua kama ile ifanyike lakini isiwe kwa kuchukiana  bali kwa kulenga umakini ili Simba ifanikiwe kwa kushinda na baada ya kazi maisha yanaendelea vizuri tu wala hakuna shida, anataka mmoja akizingua afahamishwe kwamba amezingua na ujumbe umfikie vizuri ila usimfikishie bila kumpa kipi alitakiwa kukifanya.


HATAKI PASI ZA NYUMA


Kwenye mazoezi kosa ambalo utamchukiza kocha huyo ni wakati timu inakwenda mbele basi aone mchezaji wake anarudisha mpira nyuma kwa kupiga pasi ya nyuma hapo lazima avue kofia yake na jambo moja nikuongezee kama ameshaanza kushika maneno ya kiswahili...’cheza’, ‘twende mbele’, ‘kaba’, hayo yanasikika vizuri kinywani mwake.


VIWANGO VYA WALIOANGUKA


Kuna wachezaji walionekana kama ndio basi tena Simba hebu vuta picha ya Winga Willy Onana wakati anaanza ligi ilionekana kama dirisha dogo hatoboi, muangalie Israel Mwenda, hivi sasa hata Luis Miquisson anaonekana. Hawa ni wachezaji ambao walionekana kama wataondoka haraka lakini amewarudisha na kuanza kuonekana.


Benchikha ametoa nafasi kwa wachezaji wote kasoro Aubin Kramo ambaye ni majeruhi.


SIMBA INAPATA MATOKEO


Chini ya Benchikha Simba inacheza kwa malengo ‘Objective football’ na imepoteza mechi moja dhidi ya Wydad baada ya hapo ameshinda tu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad