Kocha Gamondi: Tatizo Yanga Lipo Hapa

 

Kocha Gamondi: Tatizo Yanga Lipo Hapa

Wakati wadau wa soka wakiamini Yanga ina kikosi bora, kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amevunja ukimya akisema kina tatizo ambalo linaweza kumalizwa na wachezaji wasiopata namba kubadilika kila wanapopewa nafasi ya kucheza, vinginevyo itazidi kumpa ugumu mbeleni.


Kocha huyo amesema haridhishwi na uwezo wa baadhi ya wachezaji hasa wasiocheza mara kwa mara akikiri kuwa ana kikosi bora, lakini kisicho kipana na hilo ndilo tatizo.


Gamondi alisema kutokana na kuwatumia wachezaji wengi wanaokaa benchi katika michuano ya Mapinduzi akiamini watacheza kwa kiwango bora tofauti na walichofanya.


“Kumekuwa na maneno mengi kuwa sifanyi mabadiliko ya kikosi kwa wachezaji. Nilianza kufanya hivyo nilipata matokeo mabaya dhidi ya Ihefu FC katika mechi ya Ligi Kuu tulipofungwa mabao 2-1. Nilipoona matokeo sio rafiki nikaendelea na mfumo wangu mashabiki waliendelea kuzungumza,” alisema.


“Kwenye Mapinduzi nimetoa nafasi kwa wachezaji wote kucheza, lakini sioni wakipambana. Sina budi kusema ni kweli nina kikosi bora, lakini sio kipana. Hii ni kutokana na ubora wa wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza kuwa juu zaidi kuliko ninaowatumia kwenye mashindano haya.”


Gamondi alisema wachezaji wanashindwa kujituma na hawapambani kama matarajio ya wengi yalivyo, hivyo ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kila mmoja anawajibika ili kuipambania timu.


Wakati Gamondi akisema hayo Mwanaspoti linakuletea kikosi kwa kila nafasi kilivyo na wachezaji wa kutosha kuweza kuipambania timu.


Yanga ina makipa watatu Djigui Diarra, Metacha Mnata na Abuutwalib Mshery na msimu huu wote wamepata nafasi ya kucheza, lakini kipa namba moja ndiye aliyecheza dakika nyingi zaidi. Hivyo ni wazi kuwa Diarra ndiye kipa wa kutumainiwa tangu alipotua chini ya Nasreddine Nabi na amekuwa chaguo la kwanza huku Metacha na Mshery wakipata nafasi akikosekana.


Eneo la beki namba mbili Nabi alikuwa akimtumia Djuma Shaban ambaye alivunjiwa mkataba na alikuwa akichuana na Kibwana Shomari aliyekuwa panga pangua ambaye sasa anasugua benchi mbele ya Attohoula Yao aliye panga pangua chini ya Gamondi kutokana na ubora.


Licha ya Yao kuwa bora zaidi eneo hilo akikosekana Gamondi amekuwa akimtoa Dickson Job eneo analocheza na kumtumia pembeni eneo ambalo Kibwana anacheza, na kumuacha akiendelea kukaa benchi.


Kwa beki ya kushoto limekuwa likitumiwa kikamilifu na Joyce Lomalisa anayeendelea kuwa chaguo la kwanza akitumiwa zaidi tofauti na msimu uliopita ambao alikuwa anabadilishana na Kibwana ambaye anaweza kucheza beki mbili na tatu.


Mbali na wawili hao pia kuna Nickson Kibabage aliyesajiliwa msimu huu kutoka Singida amekuwa akicheza chini ya Gamondi tofauti na Kibwana.


Mabeki wa kati wameendelea kutumika Ibrahim Bacca, Dickson Job na Bakar Mwamnyeto, huku Gift Fred akiibua mijadala kutokana na uwezo anaouonyesha kwenye Mapinduzi, japo kwenye ligi hatumiki chini ya Gamondi tofauti na wenzake.


Eneo la kiungo ndilo lenye wachezaji wengi na mabadiliko makubwa yamefanyika chini ya Gamondi.


Kiungo mkabaji Khalid Aucho ndiye pekee aliyejihakikishia namba, huku Mudathir Yahya akionekana kusuasua na kupoteza makali tofauti na chini ya Nabi.


Pia kuna Zawadi Mauya kapoteza nafasi kwani amepata dakika chache kwa sasa, changamoto anazokutana nazo pia kiungo mshambuliaji Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye sasa hana nafasi ya kucheza mara kwa mara. Eneo hilo limekuwa likitumiwa na Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki ambaye chini ya Nabi hakuwa na namba ya uhakikika mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ (aliyehamia Azam) lakini sasa amekuwa bora.


Maxi Nzengeli aliyesajiliwa akiwa bora amemuondoa Jesus Moloko kikosi cha kwanza. Moloko anayecheza eneo la winga sambamba na Farid Mussa wamepoteza namba kikosi cha kwanza chini ya Gamondi ambaye ni muumini wa kutumia viungo zaidi na sio mawinga.


Farid licha ya kutumika maeneo mengi chini ya Nabi na kufanya vizuri sasa anaishia benchi. Eneo la ushambuliaji ambalo chini ya Nabi lilikuwa bora likiongozwa na Fiston Mayele aliyetimka kikosini pia kulikuwa na Clement Mzize na Keneddy Musonda ambao kwa sasa wameonekana kuwa butu.


Chini ya Nabi licha ya kuwa na imani kubwa na Mayele kulikuwa na mabadiliko yaliyokuwa yanafanyika kwa Mzize na Musonda kupata nafasi wakicheza kwa ubora, lakini sasa imekuwa tofauti.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad