Kocha Nabi Afika Bei Kwa Mabeki Bara, Henock Inonga


Mabeki wakali wa kati katika Ligi Kuu Bara, Henock Inonga wa Simba na Ibrahim Bacca wa Yanga wameonyesha maajabu ndani na nje ya nchi na sasa Klabu ya FAR Rabat inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasrredine Nabi imefika bei.

Subiri kidogo. Far Rabat inachekecha kati ya mabeki hao ni yupi imnyakue, lakini ukweli ni kwamba chama hilo la Nabi halina shida katika ishu ya mkwanja na ni kama liko tayari kutoa fedha zitakazotajwa iwapo mazungumzo yatafikiwa.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba upo mjadala mzito ndani ya FAR Rabat ya Morocco kuhusiana na mabeki wawili wa kati wa Simba na Yanga.

Uongozi umepania kuanza na kumaliza mchakato wa Henock Inonga wa Simba ndani ya saa 48 zijazo, lakini kocha Nasreddine Nabi anatamani kumpata Ibrahim Bacca.

Lakini, kwa hali ilivyo hana namna. Amesisitiza kuwa atakubaliana na uamuzi wa uongozi na ataweka mzigo kwa Inonga ambaye ni roho ya Simba na DR Congo.

Iko hivi. Zimesalia saa 48 tu ili usajili wa dirisha dogo kufungwa huko Morocco, huku Inonga akiwa Ivory Coast katika michuano ya Afcon ambapo kikosi chake kitakiwasha na Guinea kwenye robo fainali.


Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema tangu aanze kufundisha timu hiyo alikuta viongozi wana mawasiliano na Mkongo huyo na wanamuelewa kwelikweli sababu mbalimbali.

Alieleza kwa sasa kikosi hicho kinahitaji sana beki wa kati tena mwenye ubora baada ya aliyekuwepo Arsene Zola kuondoka, lakini Inonga ameachiwa nafasi pia kuamua.


“FAR Rabat inataka kukamilisha dili hilo ndani ya siku tatu kutoka leo ili kuwahi usajili wa dirisha dogo ambao utafungwa Jumatano saa sita usiku,” alisema Nabi ambaye pia aliwahi kuifundisha Yanga.

“Ninachohitaji sasa ni beki wa kati ambaye ni bora na mwenye uzoefu hivyo nasubiri viongozi watakachokifanya ili kukamilisha mahitaji yangu.”

Aliongeza kuwa kama ingekuwa ni uamuzi wake kuchagua beki gani asajiliwe katika kikosi hicho alichoanza kukifundisha msimu huu baada kutoka Yanga, basi angemnyakua Bacca, lakini viongozi na maskauti ya klabu wana vigezo vingi.


“Viongozi wanataka sana wachezaji wanaotoka mataifa yanayozungumza Kifaransa ili iwe rahisi kwa mawasiliano. Ila kama ningepata nafasi ya kuchagua ningemchagua beki wa Yanga Ibrahimu Bacca,” alisema Nabi aliyefundisha Yanga kwa misimu miwili mfululizo na kutwaa makombe Ligi Kuu, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Azama na kushika nafasi ya pili Kome la Shirikisho Afrika.

Huenda matamanio ya kocha huyo yakawa na usahihi, kwani anaweza kumfahamu Bacca zaidi na aina yake ya uchezaji kuliko Inonga ambaye hajawahi kumfundisha ila kamuona uwanjani alipokuwa akikutana na Simba.

Licha ya kiwango bora alichoonyesha katika michuano ya Afcon na juzi kuwa miongoni mwa wachezaji waliotupia bao la penalti katika mchezo dhidi ya Misri, ugumu unaweza kuwa kwenye mkataba mrefu alionao Simba ambayo haipo tayari kumuachia kwa sasa ingawa fungu la Waarabu linaweza kuamua.

Klabu kutoka Kiarabu zimewahi kuwang’oa mastaa wa Simba, Luis Miquissone na Clatous Chama ingawa maisha yaliwashinda wakarejea.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad