Maandamano Chadema: Ugumu wa maisha watawala




Ugumu wa maisha unaotokana na kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu, umeteka maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Maandamano hayo ya amani yasiyo na kikomo yameanza leo tarehe 24 Januari 2024, jijini Dar es Salaam, ambapo Chadema inaishinikiza Serikali kutafuta mwarobaini wa changamoto hiyo.

Katika msafara wa maandamano ulioongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kuanzia Buguruni hadi ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), zilizopo jijini humo, wananchi walijipanga mstari barabarani kuwashuhudia, huku wengine wakipaza sauti kuelezea changamoto zinazowakabili.

Kila walipopita wananchi waliokuwa pembeni baadhi yao waliokuwa wakipaza sauti wakisema “maisha magumu sana…sukari imepanda bei…wenye nyumba wamepandisha Kodi.

“Wajane tunahangaika maisha ni magumu kwetu tunanyanyasika… sukari imepanda bei mafuta yamepanda bei na Rais ananyamaza,” walisikika baadhi ya wananchi ambapo hawakuwemo katika msafara wa maandamano.

Wananchi hao waliiomba Chadema ifikishe kilio chao serikalini juu ya ugumu wa maisha, huku wakikazia ongezeko la bei ya mafura na sukari.

Mwajuma Ramadhan, aliyejitambulisha ni mkazi wa Vingunguti, alisema “Bora walivyoamua kuandamana huenda Serikali itasikia vilio vyetu maana maisha magumu sana, sukari tunanunua kilo 5,000 watoto wetu wanashindwa kunywa chai,” amesema.


Mbali na madai ya Serikali kuondoa ugumu wa maisha, Chadema inaitaka ikamilishe mchakato wa upatikanaji katiba mpya.

Pia, Chadema inaitaka Serikali iuondoe bungeni miswada ya Sheria za uchaguzi ili ifanyiwe marekebisho kwa ajili ya kujumuisha maoni ya wadau juu ya maboresho ya mifumo ya uchaguzi.

Wakati wa maandamano hayo yaliyoanza majira ya saa 10.30 kwa upande wa Buguruni, Magari yalilazimika kupitia barabara za mitaani baada ya barabara kubwa watu kujaa.

Hadi majira ya saa 13.15 mchana msafara wa Mbowe ulikuwa umefika maeneo ya Shekilango, wakiusubiri msafara wa pili uliotokea Mbezi Mwisho ambao unaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, ili wajumuike pamoja kwenda ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), kufikisha malalamiko yao.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, UN imekubali kuwapokea kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko yao

Chadema kimedai hakitaacha maandamano hadi madai yao yatakapofanyiwa kazi ikiwemo miswada inayolalamikiwa itakapoondolewa bungeni.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad