Zanzibar. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ameyakataa masharti yaliyotolewa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili washiriki mdahalo kati ya vyama hivyo viwili, akidai utekelezaji wake utavunja sheria za nchi.
Makonda amesema viongozi wa Chadema ni watu wazima wamepima kuhusu mchakato huo na njia pekee ya kuchomoka katika mdahalo ni kutoa masharti ambayo wanajua hayatekelezeki, na yeye hawezi kuwa sehemu ya wavunja sheria za nchi.
Miongoni mwa masharti yaliyowekwa na Chadema ni Serikali iondoe kwanza miswada mitatu waliodai ni mibovu bungeni inayohusu sheria za uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa, Serikali ianzishe mara moja mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 na Serikali iwasilishe bungeni muswada wa Sheria ya kukwamua mchakato wa Katiba mpya ukiwa na jibu la lini itapatikana.
Masharti hayo yalitolewa kujibu kile kilichoelezwa Jumapili, Januari 14, 2024 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akiwa Unguja Zanzibar, akitaka kufanyike mdahalo wa wazi kati yake na viongozi wa Chadema ili Watanzania wachague ikiwa wataendelea na maandamano au kuchagua maridhiano.
Leo Jumanne, Januari 16, 2024 wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi kuu ya chama hicho, mjini Unguja Zanzibar, Makonda amesema, “Chama kinachoongoza kwa demokrasia na utawala bora, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan anayeongoza kwa kuchukua tuzo, hakiwezi kuvunja sheria kama ambavyo wanataka Chadema.
“Hivi wewe ni nani uende ukatoe muswada bungeni au kuahirisha Bunge? Hoja zipo wazi wao wanataka tuwe na wabunge 740 maana ukumbi wa Bunge uvunjwe na kujenga mwingine, hivi kwa hali ya sasa tunahitaji kujenga jengo jipya kweli? Yaani tuongeze ili watu wakalale mule,” amesema Makonda.
Makonda amesema kwa hoja walizonazo CCM kabla ya Chadema kupeleka watu, wakae katika meza kwa ajili ya mdahalo ili Watanzania wasikie na kufanya uamuzi. Amesema sio kweli kwamba Serikali imekataa mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi.
“Hili jambo nitalitafutia tu muda, lakini kwa sasa chama kipo ‘busy’ kimempokea Katibu mkuu wetu (Dk Emmanuel Nchimbi na tunataka kuanda mapokezi makubwa hapa Unguja na pale Lumumba (jijini Dar es Salaam) na Dodoma kisha kumpa nafasi ya kujenga sekretarieti ya chama,” amesema Makonda.
Makonda amedai mabadiliko yaliyofanyika jana Jumatatu Januari 15, 2024 ya kumteua Dk Nchimbi kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Daniel Chongolo yamewaumiza baadhi ya vyama vya upinzani. Katika hatua nyingine, Makonda amewataka wananchi wa Unguja kujitokeza kwa wingi kuanzia kesho Alhamisi Januari 17, 2024 katika ziara ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan atakayefanya ziara katika mikoa ya minne ya Unguja.
Makonda amesema ziara hiyo ya kichama ina lenga kukagua uhai wa chama hicho na miradi ya maendeleo.
“Ratiba hii inaanza kesho (Jumatano Januari 17) hadi Januari 18 ni habari njema kwa Wana-CCM kujitokeza katika ziara hii ya siku mbili, tutaanza na Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Unguja na Mkoa wa Magharibi,” amesema Makonda.