Mambo Yanayofanya Wanawake wa Siku Hizi Washindwe kuolewa

 

Mambo Yanayofanya Wanawake wa Siku Hizi Washindwe kuolewa

Hakuna sababu ya kujifanya mbishi, hakuna mtu anayejua kila kitu hivyo ni vyema kujifunza. Usijifanye mwamba, tenga muda wako kujifunza mambo mapya kila siku. Ndugu zangu, leo nitazungumza zaidi na wanawake lakini si vibaya pia hata wanaume wakasoma ili kwa namna moja au nyingine wajue namna ya kuishi vizuri na wenza wao.


Nimekuwa nikisisitiza sana kwenye makala zangu, wapendanao wanapaswa kwenda sawa ili waweze kudumu katika safari yao. Mmoja anapokwenda kivyake, uhusiano hauwezi kuwa imara. Hakuna mwanadamu aliyekamilika, lakini yapo mambo ambayo wanawake wengi wamekuwa wakiyaamini kwa kujua au kutokujua na kujikuta wakishindwa kuingia kwenye ndoa.


Wanawake wengi ambao huajiriwa au wanajimudu kifedha, wanapokuwa kwenye suala la uhusiano huwa wanapata kiburi fulani hivi cha kujiona hivyo kujikuta wakishindwa kuishi vizuri kwenye mahusiano.


Wanashindwa kutofautisha kazi na masuala ya uhusiano. Kumbe basi, mwanamke anayejua wajibu wake, anapokuwa kazini anafanya kazi lakini akirudi nyumbani anawajibika kama mke wa mtu. Wanawake wanaoamini kwamba wanajimudu kifedha wanafikiri kwamba wapo sawa na wanaume, kuna wakati wanajisahau na kufikiri kwamba wanaweza pia kuoa wanaume jambo ambalo si sahihi kwa tamaduni zetu.


Wanawake wanaothamini kazi kuliko maisha yao ya uhusiano wanakosea. Inapaswa mwanamke ujue kwamba unafanya kazi lakini usisahau hata kidogo kumkumbuka mwenzi wako, kumuandalia mahitaji yake muhimu ili akuone upo na unamthamini kila wakati.


Wapo pia wanawake ambao wanafeli kwenye mahusiano yao kwa kuamini tu hakuna wanaume waoaji hivyo hata kama mwanamke yupo kwenye uhusiano, anaamini tu ni uhusiano wa kupita maana hakuna wanaume wa kuoa.


Ndugu zangu, mnapaswa kuepukana na imani hiyo potofu. Ishi na mtu unayeamini ni mtu sahihi kwako, achana na dhana ya kwamba waoaji hawapo kama unahisi uliyenaye si muoaji basi ni bora kuachana naye na ukaanzisha safari na mtu ambaye unamuona ni sahihi.


Wapo wanawake ambao pia wanafeli kuolewa kwa sababu tu ya kusaka mtu mwenye kipato. Nani kakwambia kipato ndio kila kitu? Unaweza kupata mtu ana kipato lakini kumbe akawa na tabia mbaya ambazo zitakugharimu maisha yako yote. Eti unamtaka mwanaume ambaye sijui ni msomi, elimu pekee haiwezi kukusaidia au kukupa furaha ya mahusiano au maisha yako. Unapaswa kuwa na mtu ambaye mtaelewana, mtaheshimiana, mtajaliana katika kila hali.


Si lazima awe tajiri au masikini, fedha zinatafutwa. Kikubwa ni utu hivyo ni bora umpate mtu ambaye ni wa kawaida, muamue tu nyinyi wenyewe mnataka kuishi maisha ya aina gani na mwisho wa siku kuyatafuta.Kama mnataka kuwa matajiri mtafuata kanuni za kujikwamua, hatimaye mtakuwa matajiri huku pia mkifurahia maisha yenu ya uhusiano.


Kuna suala la haki sawa, wanawake siku hizi wanataka haki sawa na kusahau kabisa asili au mpango wa Mungu katika suala la ndoa. Kiasili kila mtu ana majukumu yake, mke atabaki kuwa mke na mume atabaki kuwa mume. Mke atekeleze majukumu yake na mume afanye yake ili muweze kuishi vizuri.


Mke amheshimu mume, mume ampende sana mkewe na kila mmoja amthamini mwenzake!

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad