Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi mjanja sana. Baada ya kugundua kuna uwezekano wa kupigwa Kariakoo Derby katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 ameamua kuwaita nyota wake wote wa kikosi cha kwanza aliokuwa amewapa mapumziko mafupi akiwamo Pacome Zouzoua.
Mbali na Pacome aliyekuwa ameitwa kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Ivory Coast ambao ni wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zinazoanza wiki ijayo, pia kuna Khalid Aucho na Yao Kouassi aliowataka haraka kambini kujiandaa na mechi zijazo za mtoano za Mapinduzi.
Yanga ni moja ya timu nane zilizofuzu robo fainali na itacheza na APR.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji hao wametakiwa kurudi na kuungana na timu kabla ya kesho kutoka kwenye mapumziko waliyopewa ikiwa ni maandalizi ya mechi za nusu fainali iwapo timu hiyo itatoboa kesho kwenye robo fainali.
“Nafikiri Jumapili (kesho) wachezaji wote ambao hawajaitwa timu zao za taifa watakuwa wameungana na wenzao tayari kuongeza nguvu kikosini kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi ambayo imefikia patamu,” kilisema chanzo kilichoomba kuhifadhiwa jina.
“Kila mchezaji ana taarifa hii, hivyo kama kutakuwa na mabadiliko itafahamika baadaye lakini kwa mujibu wa taarifa zilizopo ndani ya uongozi ni kwamba Pacome na wenzake wote wanatakiwa kuripoti kambini mapema.”
Yanga ni moja ya timu inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la michuano hiyo kwa msimu huu wa 18 unaoenda sambamba na maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964, kutokana na aina ya kikosi ilichonacho, japo kwenye michuano hiyo imetumia zaidi wachezaji wa kikosi cha pili na wale wa vijana na wapya waliosajiliwa akiwamo Shekhan Ibrahim Khamis na Augustine Okrah aliyecheza kwa mara ya kwanza juzi usiku na kuumia kiasi cha kulazwa hospitali.
Mara ya mwisho Yanga kubeba taji la michuano hiyo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Mlandege ya Zanzibar ni mwaka 2021 ilipoifunga Simba kwa mikwaju ya penalti, likiwa ni la pili tangu Kombe la Mapinduzi lilipoasisiwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2007.
Timu hiyo ina nafasi ya kukutana na Simba kwenye hatua ya fainali kama sio nusu fainali iwapo zote zitavuka na kukumbushia Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana na kuwashindilia watani zao hao kwa mabao 5-1, Pacome akifunga bao la tano kwa mkwaju wa penalti.
Wengine waliofunga kwenye mchezo huo uliomfuta kazi kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ni Maxi Nzengeli aliyefunga mawili na Kennedy Musonda aliyepiga bao la kwanza kabla ya Kibu Denis kuisawazishia Simba kabla ya mapumziko