Mchezaji Clatous Chama Ngoma Ngumu Simba

 

Mchezaji Clatous Chama Ngoma Ngumu Simba

Kamati ya Nidhamu ya Klabu ya Simba SC iliyokuwa imepanga kusikiliza kesi inayowahusu viungo wa timu hiyo, Clatous Chama na Nassor Kapama kwa njia ya mtandao kupitia Zoom, imekwama, hivyo kufanya kesi hiyo kuendelea kusubiriwa na wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kongwe.


Chama yupo kwenye kambi ya timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ inayojiandaa na michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 na ilielezwa angeungwanishwa na wajumbe kwa Zoom ili kusikiliza na kutoa utetezi kwenye kesi hiyo inayomkabili.


Chama na Kapama walisimamishwa na uongozi tangu Desemba 21 mwaka jana kwa kosa la utovu wa nidhamu, ikidaiwa Mzambia huyo alimtolea lugha ya matusi kocha wa viungo, Kamal Boudjenane wakati timu hiyo ikipasha viungo kabla ya kuivaa Wydad katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Kwa upande wa Kapama, inadaiwa hakuhudhuria mazoezini mara kadhaa ikielezwa anashinikiza kuondoka kwasababu hapati nafasi ya kucheza kikosini.


Kamati hiyo iliyo chini ya Kamanda Mstaafu wa Polisi, Suleiman Kova, ilipanga kufanya kikao hicho Januari 3 mwaka huu, na ndipo utolewe uamuzi dhidi ya wachezaji hao, lakini kikao kilikwama.


“Kikao bado hakijafanyika, maana kikifanyika lazima yale yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho yapelekwe katika Bodi ya Wakurugenzi ndipo uamuzi ufanyike kutokana na kupitia maelezo ya wachezaji hao baada ya kuhojiwa na kamati,” amesema mmoja wa Wajumbe wa Bodi wa klabu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina na kuongeza;


“Haijajulikana ni lini, maana hili ni jukumu la Kamati ya Nidhamu ambayo ndiyo inaamua wakae lini kuwahoji wachezaji hao, kwenye Bodi ni hatua ya mwisho kuyapitia na kubariki au kutobariki kilicholetwa.”


Hata hivyo ilipotafutwa Kamanda Kova ambaye awali alinukuliwa akitaka waulizwe viongozi wa Simba SC ambao pia walisema suala hilo lipo kwenye Kamati ya Nidhamu, hata hivyo mara kadhaa alipotafutwa Kova, simu yake iliita pasipokupokewa hata ujumbe mfupi wa simu haukujibiwa

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad