Mshambuliaji wa Yanga, Chrispin Ngushi licha ya kutokuwa na nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hicho, lakini kwenye usajili wa dirisha dogo unaoendelea hivi sasa amegeuka lulu.
Baadhi ya timu za Ligi Kuu zinapishana kwenda kuiomba Yanga iwape Ngushi kwa mkopo, hivyo kuna mapambano makali ya kuwania saini yake na yenye mkwanja mrefu itafanikiwa kupata huduma yake.
Hadi sasa timu ambazo zimeifuata Yanga kuhitaji huduma ya Ngushi ni JKT Tanzania, Geita Gold na Mtibwa Sugar.
Kiongozi mmoja wa Mtibwa Sugar (jina tunalo), amekiri kuwa kwenye mazungumzo na mchezaji huyo ambayo yamefikia asilimia 80.
"Jambo la kwanza tuliiandikia barua klabu yake kumuomba kwa mkopo. Hatua ya pili kuna kiongozi mwenzetu alimfuata mchezaji mwenyewe kwenda kuzungumza naye Zanzibar, ambako Yanga ilikwenda kucheza Kombe la Mapinduzi," amesema kiongozi huyo.
Hadi sasa Yanga imecheza mechi 11 za Ligi Kuu Bara, lakini kati ya hizo Ngushi ametumika kwa dakika 11 pekee dhidi ya Mtibwa.
Ili Ngushi aweze kukinusuru kipaji chake amepewa ushauri na staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel aliyeeleza kwamba bado ana umri wake unamruhusu kucheza kwa muda mrefu.
"Nilikuwa naye Mbeya Kwanza ambako nilikuwa meneja wa timu. Ni mchezaji mwenye kasi, pumzi na nguvu. Kukosa nafasi ya kucheza Yanga siyo mwisho wa uwezo wake, atoke. Akionyesha uwezo wake anaweza akarejea tena," amesema Gabriel.
"Mbona kuna wachezaji wengi waliondoka baada ya kufanya vizuri walikokuwa wakarejea tena? Ajiamini apambane kwa sababu ndio kazi yake."
Wakati Gabriel akitoa ushauri huo kwa Ngushi, jana Rais wa Yanga, Hersi Said alikaririwa akisema timu hiyo haitakuwa na nafasi ya kuencelea kubaki na mchezaji ambaye hachezi mara kwa mara na kwamba, itawafungulia mlango wote wasio na namba ili wakatafute masiha mapya sehemu nyingine.