Mdude adaiwa kukamatwa Namanga, Uhamiaji wafuatilia



Mdude adaiwa kukamatwa Namanga, Uhamiaji wafuatilia


Jeshi la Uhamiaji limesema linafuatilia taarifa za askari wake kudaiwa kumkamata mwanaharakati, Mdude Nyagali katika mpaka wa Namanga akielekea nchini Kenya.


Taarifa za madai ya kukamatwa kwa mwanaharakati huyo, zilisambaa katika mtandao wa X (zamani Twitter), zikichapishwa na Wakili Peter Madeleka.


Katika ukurasa wake wa X, Madeleka ameandika, “Mwanaharakati Mdude amekamatwa na Uhamiaji katika mpaka wa Namanga alipokuwa anaelekea Kenya kwa madai eti ana kesi ya uhaini kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Namanga. Kwa kuwa Mdude sio mkimbizi natoa wito aachiwe haraka.”


Alipotafutwa n kufafanua taarifa hiyo leo, Jumatatu Januari 29, 2024 Madeleka amesema taarifa ya kukamatwa kwa mwanaharakati huyo ameipokea kutoka kwake mwenyewe katika mpaka wa Namanga akielekea nchini Kenya.


Ameeleza sababu aliyoelezwa kuwa chanzo cha kukamatwa kwake ni kesi ya uhaini anayodaiwa kuwa nayo, ingawa kwa mujibu wa Madeleka haijulikana ya lini.


“Wamemwambia ana kesi ya uhaini, mimi na wewe hatujui hiyo kesi ya lini na juzi Mdude alikuwa Dar es Salaam kwenye maandamano ya Chadema kwa nini hakukamatwa hapo,” amehoji Madelaka.


Hoja nyingine iliyoibuliwa na Madeleka ni utaratibu wa kisheria kuhusu kesi ya uhaini, akisema kwa kawaida kesi hizo huwa hazina dhamana imekuwaje Mdude alikuwa nje.


Mbali na hoja kuhusu kesi inayodaiwa kusababisha kukamatwa kwake, Madeleka amesema kwa kuwa mwanaharakati huyo ni binadamu ana haki ya kutembea popote ikiwemo nje ya nchi.


Ameeleza haki hiyo inabainishwa katika Ibara ya 17 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, hivyo alikuwa na haki ya kwenda anakokwenda.


Ibara hiyo 17(1) inaeleza: “Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.”


Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Jeshi la Uhamiaji, Paul Mselle amesema anafuatilia taarifa hizo na atakuwa na majibu zaidi baada ya hapo.


“Ndiyo kwanza wewe unaniambia, sina taarifa hizo. Kwa kuwa umeniambia ngoja nifuatilie kisha nitakupa taarifa zaidi,” amesema Mselle.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad