Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imesema kutokana na maboresho na mikakati inayofanywa na Serikali kumefanikisha kuongezeka maradufu kwa meli za mizigo katika bandari mbalimbali zilizopo nchini hususan katika Bandari ya Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa (TPA) Plasduce Mbossa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu bandari hizo pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshwaji kwenye mitandao ya Kijamii zinazodai kuwa uendeshaji hauridhishi ambapo amesema katika kipindi cha miezi sita pekee meli 979 zimehudumiwa wakati matarajio yalikuwa ni meli 700.
Aidha amesema changamoto kubwa ambayo ipo hivi sasa ni gati chache na kushindwa kupokea meli kubwa zaidi kutokana na kina cha bahari na kwamba mikakati waliyonayo ni kuongeza gati katika Bandari Kuu ya Dar es salaam pamoja na bandari zingine.
Mkutano huo umeongozwa na kauli mbiu inayosema Vyombo vya Habari ni Daraja la Mawasiliano Kati ya TPA, Wateja, Wadau na Umma.