Bondia wa ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo amewatoa hofu mashabiki wa ngumi kuwa pambano lake dhidi ya Mbiya Kanku wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) litakuwepo na amejipanga kuonesha uwezo mkubwa.
Mwakinyo na Mbiya watacheza pambano la kugombania mkanda wa ubingwa wa WBO raundi 10, uzito wa kati litakalofanyika kesho Jumamosi (Januari 27) Uwanja wa Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Mwakinyo amesema yanakwenda vizuri isipokuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa na nia mbaya na kumtumia ujumbe mpinzani wake asipigane kwa lengo pambano livunjike.
Amesema wamejipanga kuonyesha mchezo ambao wengi hawajahi kuuona, akiahidi ngumi ambazo mashabiki zake watazifurahia.
“Kuna baadhi ya watu wanamtumia mpinzani wangu meseji asikubali kupamnbana, pambano liharibike ionekane kawaida yangu kuharibu mapambano kitu ambacho siyo kweli.
“Nimefanya mazoezi sana, nina hamu ya kuonyesha kile nilichokiandaa, naamini wengi watafurahia mchezo mzuri, niko tayari na imebaki asilimia chache za mimi na mpinzani wangu kupima afya lakini kila kitu kiko sawa,”amesema Mwakinyo.
Mwakinyo anapanda ulingoni akiwa na kumbukumnbu ya kushinda kwa pointi dhidi ya Kuseva Katembo kutoka Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo (DRC) pambano fililofanyika mwaka jana.
Mabondia wengine watakaozichapa katika mapambano ya utangulizi ni Hemed Pelembela dhidi ya Fikiri Mohammed kutoka Bagamoyo, Hussein Itaba dhidi ya Juma Misumari wa Morogoro, Bakari Bakari na Seleman Hamad, Masoud Khatibu na Yahaya Khamis, Debora Mwenda kutoka Mbeya dhidi ya Zulfa lddi wa Dar es salaam.