Mwananchi ilibaini uwepo wa ushirikiano kati ya wazazi na shule katika kuchanga fedha za kuwapa wasimamizi wa mitihani ili watoe mwanya wa udanganyifu na kupatikana matokeo mazuri.
“Wengi wetu tumekata tamaa na kazi. Mazingira ya kazi hayana motisha hata kidogo, ukizingatia shule zetu zinahitaji ufaulu bora. Hapa ndipo tunaposhawishika,” anaeleza mmoja wa walimu mwenye uzoefu wa miaka mingi katika usimamizi wa mitihani.
Mwalimu huyo aliyezungumza kwa sharti ya kutotajwa jina, anasema posho kiduchu ya kusimamia mitihani na mazingira magumu ya ualimu yanashawishi kukengeuka.
Mwalimu huyo anasema ushawishi wa fedha ambazo aghalabu hutolewa kwa ajili ya kuruhusu udanganyifu katika mitihani, huwa zaidi ya kima cha ujira wa kazi ya ualimu kwa mwezi.
“Baadhi yetu tunafanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo, unapata fursa ya kusimamia mtihani wa Taifa, unalipwa Sh55,000 kwa siku, Sh165,000 tu kwa siku tatu. Hapa ndipo tatizo linapoanzia,” anasema.
Kinacholipwa
Mwalimu huyo anafafanua kwa baadhi ya shule msimamizi hulipwa kati ya Sh500,000 hadi Sh1 milioni kwa ajili ya kuruhusu udanganyifu ufanyike.
“Ukikuta kikundi kilichojipanga vizuri kinakupa bahasha ya Sh500,000 au Sh1 milioni, utafanyaje? Wanachotaka usinzie au usiwe mkali au mara nyingine utoke kwenda msalani,” anasema.
Anaeleza kwa takriban dakika nne hadi tano wanafunzi walioandaliwa huenda kuchukua matokeo kwa zamu na kugawa kwa wengine wote.
Anataja tamaa ya kutaka shule ipate sifa ya kufaulisha inachangia vitendo hivyo kufanyika katika shule binafsi na hata za umma.
“Baadhi ya viongozi wa shule za umma wanahusika kwa sababu zipo shule ambazo hazitaki kushusha hadhi zao, huku ubadhirifu huo ukipangwa zaidi na baadhi ya halmashauri za manispaa zilipo shule hizo,” anasema.
Wengine waliohojiwa wamebainisha hali hiyo inachagizwa na ukosefu wa umahiri kitaaluma, tabia mbaya, wasiwasi, hofu, ufundishaji usiofaa, mpangilio duni wa viti na msongamano wa watahiniwa katika kumbi za mitihani.
Teknolojia na mazoezi
Hata hivyo, uchunguzi huo umebaini maendeleo ya teknolojia ni silaha nyingine inayotumika katika ubadhirifu huo, wengi huunda makundi ya mtandao wa WhatsApp kufanikisha shughuli hizo.
Makundi hayo hurahisisha kusambaza maswali na kuyatafutia majibu kabla ya siku ya mtihani kwa ajili ya kuyagawa wakati utakapofika.
Akizungumzia hilo, Mwalimu mkuu msaidizi katika moja ya shule zilizofanya vizuri jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa), anasema uwepo wa simu janja umeongezeka na kuleta njia mpya za udanganyifu katika mitihani.
“Sasa hivi vikundi vinaundwa mapema kabla ya muda uliopangwa wa mitihani, ujumbe mfupi wa simu unatumwa, na wakati mwingine baadhi ya maswali yanapokewa kabla hata mtihani haujasambazwa kwa shule binafsi, imekuwa rahisi na salama zaidi kwa wadanganyifu,” anasema.
Hata hivyo, anaeleza siri ya ufaulu mzuri kwa miaka mingi shuleni kwake ni kuundwa kwa kamati kati ya wazazi na uongozi wa shule kupanga njama za upatikanaji wa matokeo bora.
“Tuliwaambia wazazi wachangie Sh30,000 kila mmoja, wazazi na walezi wote 200 ambao watoto wao walikuwa watahiniwa waliitikia vema. Zilipatikana takriban Sh10 milioni na zilitumika kuwarubuni wasimamizi wakuu wa mitihani katika kituo chetu,” anafichua.
Mwalimu huyo alionyesha moja ya kundi la WhatsApp waliloanzisha baada ya kuhakikishiwa kupata maswali ya mitihani ya masomo matatu siku moja kabla ya mtihani.
“Cha kushangaza ni kwamba asilimia 90 ya maswali tuliyotumwa yalikuwepo, ndipo tukamlipa aliyetupa maswali hayo,” anafichua na kuongeza kuwa kila mkuu wa shule au mmiliki alitoa Sh200,000, huku kundi hilo likiwa na wanafunzi 30.
Hata hivyo, alibainisha, “Necta (Baraza la Mitihani Tanzania) imekuwa na nia ya dhati kwa miaka ya hivi karibuni, lakini juhudi zaidi zinatakiwa kufanyika kwa sababu wanaovujisha maswali wanapata fedha nyingi... Kwa mitihani mitatu tu, tulimpa jumla ya Sh6 milioni.”
Juhudi za Serikali
Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kutoridhishwa kwake na hali ya uvujishaji wa mitihani, katika maadhimisho ya miaka 50 ya Necta Desemba 2023. Aliitaka Wizara ya Elimu na Necta, kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wizi na udanganyifu katika mitihani.
Rais Samia alisisitiza umuhimu wa upimaji wa haki katika kujenga nguvu kazi yenye tija, huku akitaka hatua kali zichukuliwe ili kuondoa mianya inayoruhusu kujitokeza kwa wahitimu wasio na tija.
Licha ya juhudi zinazoendelea za kupunguza ubadhirifu huo, dosari zinaonekana kuendelea. Necta imetekeleza hatua za kukabiliana na udanganyifu, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa shule zilizotajwa kuwa ni vituo vya udanganyifu.
Mwaka 2022, shule 24 zilifungiwa na matokeo ya watahiniwa 2,194 yalifutwa kwa sababu ya majaribio yaliyothibitishwa ya udanganyifu. Mwaka 2023, watahiniwa 31 walifutiwa matokeo na kusababisha vituo viwili vya mitihani kufungiwa.
Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda alikiri kuwepo kwa changamoto za uvujaji wa mitihani siku za nyuma, lakini amedai kuna mafanikio katika kudhibiti hilo.
“Kilichokuwa kinafanyika ni udanganyifu wa kitaasisi, shule moja inashirikiana na baadhi ya viongozi, mtihani unafunguliwa mkoa mwingine, inapigwa picha, kisha inafungwa tena na picha inapelekwa mkoa mwingine,” alifafanua Profesa Mkenda.
Waziri huyo alibainisha baada ya jitihada mbalimbali za udhibiti zinazofanywa na kamati za mitihani za mikoa na wilaya, rushwa imedhibitiwa na majaribio hayo yamepungua kulinganisha na zamani.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa kamati ya mitihani kutoka Mkoa wa Shinyanga alibainisha pamoja na jitihada hizo, hila zimeendelea kudumu, huku akisisitiza kuwepo kwa umakini.
Alisisitiza haja ya ushirikishwaji wa idara za usalama wa Taifa na ujasusi kufuatilia na kuzuia vitendo viovu kabla.
“Uchunguzi wa kina kabla ya mitihani ya Taifa uwe unafanyika. Walengwa wawe mameneja na kamati zinazohusika na kupanga udanganyifu, unapaswa kufanywa kila wakati mwisho wa mitihani.”
Kuboresha mazingira ya kazi ya walimu, kuimarisha mafunzo na umahiri wao na kutekeleza hatua kali dhidi ya rushwa ni njia zinazopendekezwa kufanyika kutatua changamoto zilizopo.
“Kuwekeza katika teknolojia ili kuhakikisha mchakato wa mitihani na kuhusisha vyombo vya usalama vya Taifa katika ufuatiliaji makini ni muhimu ili kuzuia udanganyifu,” alisema mtaalamu wa elimu, Dk Amos Majula.
Alipendekeza mamlaka za Serikali, wadau wa elimu na jamii kwa jumla zishirikiane ili kupata suluhu madhubuti itakayokomesha changamoto za kiuchumi, mifumo ya teknolojia na utovu wa nidhamu kwa walimu.
“Ni wakati wa kulinda uadilifu wa mfumo wa elimu wa Tanzania na kupata mustakabali ambao mafanikio ya kitaaluma yataakisi ujuzi na uwezo wa vijana,” alisema Dk Majula.