Mwenyekiti SIMBA Murtaza Mangungu Awagawa Wanachama Simba
Simba ipo kwenye mchakato wa kufanya marekebisho ya Katiba kama ilivyoelekezwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), huku maoni mengi ya wanachama yaliyotumwa kwenye Kamati Maalumu iliyoundwa kusimamia mchakato huo ikiikomalia nafasi ya Mwenyekiti wa klabu inayoshikiliwa kwa sasa na Murtaza Mangungu kwenye uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi.
BMT iliielekeza Simba kufanya marekebisho hayo baada ya kugundua ina upungufu uliochangia kukwamisha kukamilika kwa mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya Simba iliyo chini ya Mwenyekiti, Wakili Hussein Kita, Makamu Mwenyekiti Wakili Aziza Omary na wajumbe watano ilikutana mara kadhaa kupitia maoni ya wanachama wao juu ya marekebisho hayo, lakini kubwa kati ya maoni yote ni nafasi ya mwenyekiti wa klabu ndani ya Bodi ya Wakurugenzi.
Hivi sasa mwenyekiti wa klabu ya Simba ni Murtaza Mangungu ambaye Katiba yao ya toleo la mwaka 2018 haimpi nguvu ya kufanya uamuzi wowote kwenye Bodi hiyo.
Katiba ya Simba haijafafanua juu ya majukumu ya Mwenyekiti wa klabu anayechaguliwa na wanachama, kwani Ibara ya 29 kwenye Muundo wa Bodi ya Wakurugenzi, kipengele cha kwanza inasema ‘Klabu ya Simba itafanya kazi chini ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Sports Club Company Limited’.
Maoni mengine ambayo yameonekana kutolewa kwa wingi na wanachama wa Simba ni kolamu ya idadi ya wanachama kwenye mkutano mkuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Wakili Kita alisema baada ya mchakato huo wa awali, sasa kamati yake inaandaa Rasimu ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wanachama wao kabla ya mkutano mkuu kufanyika Januari 21, mwaka huu.
“Kwenye mkutano mkuu wanachama wote wataijadili hiyo rasimu, kama wataipitisha ama kutakuwepo na nyongeza nyingine basi itajadiliwa siku hiyo, ndipo tutaipeleka rasimu kwa msajili, maoni yalikuwa mengi... sasa ni utekelezaji tu,” alisema Wakili Kita.