Ndege ya ATCL yapakia tani 51 za mizigo Nairobi siku mbili baada ya kumalizika mvutano




Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Serikali ya Tanzania na Kenya kumaliza tofauti iliyokuwepo katika huduma za usafiri wa anga, Ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Tanzania jana imefanya safari yake ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Dubai kupitia Nairobi.

Taarifa zilizothibitisha zinaeleza kuwa ndege ya ATCL aina ya Boeing 767-300F jana iliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi, Kenya baada ya Tanzania na Kenya kukubaliana kuondoa vikwazo vya biashara kwenye Sekta ya Anga.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kupakia tani 54 ilitokea Dar es Salaam ikiwa tupu, ilipakia mizigo yenye uzito wa tani 51 kwenda Dubai katika Falme za Kiarabu ikiwa ni safari yake ya kwanza katika kituo hicho.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amethibitisha kuwepo kwa safari hiyo na kuwa ndege hiyo iliondoka jijini Nairobi, saa 3:30 na kuwasili Dubai saa 8:28 usiku 18, Januari 2024 na inatarajiwa kurejea nchini leo Januari 19, 2024.

Aidha ndege hiyo ya mizigo iliyowasili nchini Juni 2023 ilifanya safari yake ya kwanza kwenda Dubai ikitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) Julai 2023 na imekuwa ikifanya safari za ratiba kati ya Dar es Salaam na Mumbai, India.

Nchi nyingine ambazo huwa inachukua na kupeleka mizigo ni Lusaka (Zambia), Harare (Zimbabwe) pamoja na Lubumbashi na Kinshasa (DRC).

Januari 15 Mamlaka ya Usafiri wa anga ya Tanzania (TCAA) ilitangaza kusitisha kibali cha Shirika la Ndege la Kenya (KQ) ikiwa ni hatua ya kujibu hatua iliyochukuliwa na mamlaka za anga la Kenya kukataa maombi ya ATCL ya kufanya safari za ndege ya mizigo kati ya Nairobi na nchi nyingine.


Mvutano huo uliwasukuma Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya kufanya mazungumzo haraka ambayo yalimaliza jambo hilo siku iliyofuata kwa Kenya kutoa vibali kwa ATCL na TCAA kurejesha kibali cha KQ.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad