Akatambulishwa Augustine Okrah juzi katika Uwanja wa Amani pale Zanzibar. Kwamba kuanzia juzi yeye ni mchezaji wa Yanga. Hii ni namna maisha yanavyokwenda kasi katika mpira wa Tanzania. Wakati mwingine maisha yetu katika soka yanakuwa kama mazingaombwe.
Alipokuja Simba Julai mwishoni 2022, Okrah alitambulishwa kama 'magician'. Kwamba miguu yake ilikuwa imejaa maajabu. Katika dirisha hilo la uhamisho ghafla Simba walionekana wamelamba dume kwa sababu mbalimbali. Wengine tulikwenda kupekua katika makabrasha na kugundua mambo mawili ambayo yalitufanya tuwasifu Simba.
Kwanza alikuwa mchezaji bora zaidi katika Ligi Kuu ya Ghana. Pili ikagundulika kwamba alikuwa miongoni mwa wachezaji wachache sana wanaocheza ndani ya Ghana ambao huwa wanaitwa katika timu ya taifa. Ni ngumu kwa mchezaji wa ndani kutoka katika mataifa ya Ghana, Nigeria, Cameroon, Mali au Senegal kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa.
Kwanini? Hawa jamaa huwa wana wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi zao. Wapo wanaocheza Ulaya, Afrika, Asia, Australia na kwingineko. Anapoteuliwa mchezaji kutoka ligi ya ndani, basi lazima awe na kitu maalumu. Makipa huwa wanapata fursa hiyo kwa sababu nchi hizi hazipeleki makipa wengi Ulaya na kwingineko.
Ni wazi kwamba Simba walionekana wamelamba dume kwa Okrah. Alipotua na kuanza kucheza tuliona cheche zake. Kipaji kilikuwa pale kwa kila mtu kuona. Baada ya hapo kilichofuata kilikuwa historia. Wote tunafahamu kwamba Okrah hakuwika Simba. Muda mwingi aliutumia nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja.
Kuna wakati alikuwa majeruhi halafu kuna wakati akaonekana kama vile amepona lakini alikuwa na matatizo na uongozi. Kuna wakati tukaambiwa kuwa nidhamu yake ilikuwa mbovu. Tatizo ni kwamba uongozi wa Simba haukuwahi kujitokeza hadharani na kuweka wazi matatizo ya Okrah. Mashabiki na waandishi wa habari walibaki kukisia tu matatizo ya mchezaji na klabu yake.
Baadaye mkataba wake na Simba ukavunjwa.
Awali ilionekana kama vile alikuwa mchezaji aliyekuja nchini kuziba pengo la Luis Miquissone, lakini na yeye akaingia katika kundi la kina Peter Banda. Si kwa uwezo, bali kwa kushindwa kuziba pengo la Miquissone kwa sababu mbalimbali. Hili lilikuwa moja kati ya anguko la Simba miaka ya karibuni.
Baada ya kurudi kwao Ghana, Okrah alijiunga na klabu ya Bechem inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo. Ameuwasha moto. Katika mechi 15 alizoichezea timu hiyo amefunga mabao manane na kupiga pasi za mwisho mbili. Novemba alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ghana.
Ilitosha kuwafanya Yanga waisake saini yake na kumpa mkataba wa miaka miwili. Na sasa mashabiki na wachambuzi wamebaki wameduwaa kwa uamuzi wa Yanga kumchukua Okrah. Anayeamini kwamba wamefanya uamuzi sahihi kumchukua Okrah ni Hersi Said na watu wake wachache. Ni wao ndio wanaoweza kutuelezea vizuri kuhusu kamari hii.
Kama sio wao kwa sasa, basi muda utatuelezea vizuri kuhusu uamuzi huo. Wakati mwingine unafunga mdomo na kusubiri mambo uwanjani. Tumewahi kufanya hivyo kwa wachezaji kadhaa. Wapo waliotuziba midomo na wapo ambao walishindwa kukosoa hisia zetu. Tulionekana kuwa sahihi kwa kupinga baadhi ya uamuzi.
Mfano ni Bernard Morrison. Namna alivyowasumbua Yanga wakati anataka kuondoka. Akaenda Simba akayatenda yaleyale aliyowahi kuwafanyia Yanga. Simba walijaribu kumsafisha mwishowe akawanyea. Yanga nao wakataka kujifanya wajanja na wanaojua kuwarekebisha wachezaji wenye nidhamu tata wakamrudisha tena. Akawafanyia yaleyale ambayo alikuwa amewafanyia Simba.
Lakini kuna upande mwingine mzuri wa maisha. Kwa mfano ni suala la Saido Ntibanzokinza. Yanga waliachana naye akaenda zake Geita Gold. Akaupiga mwingi na Simba wakaamua kumrudisha mjini. Kwa kiasi kikubwa amewasaidia Simba kiasi cha kuwa mfungaji wao bora msimu uliopita. Kwa hiyo haya mambo huwa yana pande mbili.
Na sasa ni juu ya Okrah kufanya maajabu juu ya maajabu. Maajabu ya kwanza ni kuonyesha uwezo wake uliosababisha aitwe magician. Maajabu ya pili ni kuonyesha kitu ambacho hakutuonyesha alipokwenda Simba. Kwamba apate mafanikio makubwa akiwa na Yanga. Mafanikio ambayo yatatushangaza kwa kiasi kikubwa.
Akifanikisha hili, na nadhani ndilo alilolipania zaidi, basi kwa kiasi kikubwa atakuwa amewachonganisha viongozi wa Simba na mashabiki wao. Ni wazi kwamba mashabiki wa Simba watawajia juu viongozi kwamba hawawezi kuwatunza wachezaji wazuri na kupata ubora. Wengine wataenda mbali kwa kuamini kwamba hata kina Clatous Chama hawatendewi haki klabuni.
Kama Okrah akishindwa kuwika Yanga na kisha akaleta matatizo yaleyale ya Simba, basi tutabaki kuwacheka tu kina Hersi kama tulivyofanya katika ujio wa pili wa Morrison pale Yanga. Itakuwa ni hadithi ya kunguru kutofugika. Na tutawacheka sana kwa sababu imekuwa mazoea kwa klabu hizi kukomoana bila sababu. Yote haya yanasubiri miguu ya Okrah. Kipaji kikubwa kipo pale ni suala la uamuzi wake kufanya kazi.
Inawezekana amekwenda Ghana amefanya kazi kwa sababu alikuwa na njaa ya kutoka tena nje ya mipaka ya kwao. Wakati mwingine kuna baadhi ya wachezaji wapo hivi. Akipigwa na njaa nyumbani anapambana kuhakikisha anatoka. Akitoka anaridhika na kufanya mambo ya ajabu.
Rafiki yangu mmoja alinisimulia baadhi ya wachezaji wa Kitanzania wenye sifa hizi. Akienda Simba au Yanga anaridhika. Akienda Kagera Sugar au Coastal Union anapambana vilivyo. Tusubiri kuona kama Okra atakuwa mchezaji wa namna hii. Kwanini alifeli Simba na kwanini atafaulu Yanga? Ni swali tunalojiuliza kwa kiasi kikubwa.
Kama akifikia malengo ya kipaji chake, basi Yanga itatisha zaidi. Kama akiungana na Pacoume Zouzoua, Maxi Nzingeli, Aziz Ki, Clement Mzize na Kennedy Musonda bado Yanga itakuwa na safu ya ushambuliaji inayotisha. Lakini zaidi ni kwamba tutakiri hadharani kwamba Hersi anajua kupiga hesabu zake vyema za manunuzi ya wachezaji.
Tusubiri na kuona. Muda utatuambia. Nani anaondoka? Nauona mwisho wa Skudu Makudubela. Alikuja nchini kwa mbwembwe, lakini sidhani kama Yanga na kocha wameridhika na walichokiona. Haishangazi kuona Yanga wameanza kwa kuchukua winga. Rafiki yangu, Jesus Moloko pia nauona mwisho wake.