Baada ya kutambua kiwango cha utimamu wa mwili kwa kila mchezaji juzi kwenye fukwe ya bahari ya Hindi, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi kesho atawatesti kina Augustine Okrah na Shekhan Ibrahim waliosajiliwa dirisha doho kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Dar City ili kujua kama mambo yataenda sawa.
Yanga licha ya mastaa wao saba wa kikosi cha kwanza kuwa nje ya timu wakiwa na vikosi vyao vya timu ya taifa kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, kocha Gamondi ameendelea na maandalizi tayari kwa ajili ya kujiweka fiti kutetea taji.
Pia Yanga inakabiliwa na mechi mbili za kumalizia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazochezwa kati ya Februari 23 na Machi 1, Ligi Kuu inayotarajia kurejea mapema mwezi ujao na ASFC.
Mabingwa hao walianza mazoezi Jumatatu wiki hii, wakijifua mara mbili kando ya bahari na baada ya kocha kubaini utimamu wa mwili kwa wachezaji wake ameomba kutafutiwa mechi watakayocheza kirafuiki na Dar City imekubali kuwatesti.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi amesema wachezaji waliopo wana kila sababu ya kuweka miili yao tayari kwani kukaa nje ya uwanja muda mrefu kutampa kazi ya kuanza upya kuwajenga kiushindani.
"Leo kama ombi litakubaliwa tutakuwa na mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Dar City hii ni baada ya kuona wachezaji miili yao imeanza kukaa sawa tayari kwa ushindani na baada ya mazoezi magumu ya siku mbili mchangani," amesema Gamondi na kuongeza;
"Utimamu wa mwili kwa wachezaji upo katika hali nzuri naamini tukicheza na mchezo leo watarudisha akiri kazini na tutakuwa tayari kwaajili ya kuendelea kujiweka kwenye hali ya kiushindani mapema kabla ya mashindano kurudi."
Yanga inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara na kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi D linalongozwa na Al Ahly ya Misri. Pia ni klabu inayokamata nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu ikifunga 30, moja pungufu na iliyonayo Azam inayoongoza msimamo wa ligi iliyosimama kwa sasa.
Katika dirisha dogo, Yanga iliwatema Jesus Moloko, Hafiz Konkoni na Crispin Ngushi ili kuwapisha Okrah, Shekhan na Guede wakiwa wamebeba tumaini na kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambao ina kiporo cha mechi ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Hausing ya Njombe.