Oscar Oscar: Fei Toto ni Bora Kuliko Pacome

Oscar Oscar: Fei Toto ni Bora Kuliko Pacome


Ni vigumu sana kumpata Mfalme wa Soka la Tanzania nje ya Simba na Yanga. Ni vigumu sana. Jean Baleke anaimbwa sana kuliko Prince Dube. Hakuna ubishi. Huu ndiyo ukweli. Soka letu wafalme wote wako Simba na Yanga.


Mmoja wa wachezaji waliokuwa na mwanzo mzuri msimu huu ni kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum. Bonge moja la kiungo. Hata hivyo, hatoki Simba na Yanga. Hapa ndipo tatizo lilipo.


Huko nyuma kidogo walau kulikuwa na wafalme nje ya Simba na Yanga lakini, sio kwenye kizazi hiki. Azam FC wamekwenda mapumziko ya Krismas na Mwaka Mpya wakiwa vinara wa Ligi Kuu Bara.


Hata hivyo, wengi wanaona ni kama Tembo tu yuko juu ya mti, muda ukifika atashuka tu chini. Wamekuwa na kiwango kizuri sana na moja kati ya wachezaji wao bora ni Fei Toto. Anaupiga mwingi sana Azam Complex. Anafunga sana na kutengeneza mabao msimu huu.


Hata hivyo, baada ya yote hayo, kelele zake zinaishia Chamazi. Ubora wake wote haufiki mjini. Hakuna anayejali.


Mabao yake msimu huu angekuwa Simba au Yanga nchini nzima ingekuwa inamuimba pengine kuliko hata Pacome Zouzoua. Hili ndiyo tatizo la soka letu, hasa unapokuwa nje ya Simba na Yanga. Hakuna mtu ana shughuli na wewe. Wote wanabaki na timu zao mbili tu nchini.


Sitaki kuweka namba za mabao na pasi zilizozalisha mabao hapa. Najua kila mtu anazo na anazifahamu.


Soka ni mchezo wa wazi na kila mtu ana maoni yake tofuati. Kwa mechi hizi chache za msimu huu, mimi nadhani Pacome amekuwa bora zaidi kimataifa eneo ambalo Fei Toto na Azam FC walitolewa mapema kabisa. Huku Pacome hakamatiki lakini, kwenye ligi yetu nadhani Fei Toto bora zaidi kuliko Pacome. Ndiye mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa Azam FC kuwa kileleni hadi tunaingia Mwaka Mpya.


Maamuzi yake uwanjani yamekuwa na tija sana kwa timu. Mabao yake na pasi za mwisho zimeipa Azam FC alama tatu msimu huu. Ni mchezaji yule aliyekuwa Yanga na tegemeo kwenye timu ya Taifa. Tatizo ni moja tu safari hii, hayuko Simba na Yanga. Huku ndiko waliko Wananchi, mashabiki wa soka la nchi yetu. Fei Toto haimbwi tu lakini kwa ligi yetu ilipofikia hadi sasa, amekuwa na mchango mkubwa kuliko Pacome.


Tayari Azam FC ina pointi 31 baada ya mechi 13 za mwanzo, sio mwanzo mbaya. Mabao 35 waliyofunga na ukuta wao kuruhusu mabao 10, ni uwiano mzuri sana kwa timu. Moja kati ya mambo mazuri ya Azam FC msimu huu, ni kuona namna wanavyozidi kuongeza nguvu kwenye kikosi chao. Kama waamuzi wataendelea kutenda haki, kuna namna wanaweza kusumbua msimu huu. Waamuzi wetu nao kuna muda wamekuwa na makosa yanayoumiza kwa kiasi kikubwa timu ndogo na kuzibeba Simba na Yanga. Sio kwamba Simba na Yanga wao hawaumizwi na makosa hayo, hapana. Lakini wao ndiyo wanufaika wakuu. Ni kweli Azam FC wanaweza kutwaa Ubingwa msimu huu? Sidhani kama yupo wa kuwawekea dhamana na haÅŸa kwa kutazama moto wa Yanga na namna Simba walivyokuwa na kiu ya ubingwa. Uzuri ligi bado mbichi lakini tayari wachezaji na timu zimeshaanza kujipambanua. Tayari Fei Toto ameonyesha Ubora wake.


Tayari Yanga wanaanza kuonyesha dalili za kwenda kutetea ubingwa. Bado simba wanapambana kujipata vizuri.


Uwekezaji wanaoendelea nao Azam FC na haÅŸa wa wachezaji, ni njia bora sana. Sasa taratibu wanaanza kufikia Ubora wa wachezaji wengi waliopo Simba na Yanga. Hii ndiyo njia sahihi ya kwenda kushindana na wafalme wa soka letu.


Waamuzi wakiifanya kazi yao vizuri, TFF na Bodi ya Ligi nao wakifanya majukumu yao sawa sawa, tutampata bingwa wa kweli.


Natamani kuona Fei Toto na Pacome wanakuwa fiti msimu mzima ili nione watamalizaje.


Ni kwa kuwa tu Fei Toto hachezi timu za wafalme, ila kwa ligi ya ndani, umeupiga mwingi hadi sasa. Pacome kiuhalisia ni kama mchezaji aliyebeba maono ya Yanga. Amekuwa na maamuzi mengi yenye msaada kwa timu.


Ndiyo mtu anayeweza kubadilika haraka sana kutokana na mahitaji ya mechi na muda husika.


Hakuna ubishi, huu ni moja ya usajili bora kwa Yanga msimu huu. Lakini bado nikitazama kwa hapa ligi ilipofika, namwona Fei Toto kama mchezaji bora mbele ya Pacome. Mwishoni mwa msimu naweza kuja na maoni tofauti lakini kwa sasa, Fei Toto kwenye ligi amekuwa bora sana. Mabao na pasi zake za mwisho, vinamweka juu. Uzuri soka ni mchezo wa wazi na wa maoni. Najua na wewe unatazama na una maoni yako.


Sio mbaya kama utaamua kunitumia kupitia ujumbe mfupi wa maandishi wa namba ya simu iliyowekwa hapo juu. Hapa Pacome, pale Fei Toto. Unawaona Azam FC wakiwa kwenye mbio za ubingwa au ni Tembo mtoto tu anayeonekana juu ya mti?

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad