KIUNGO wa Yanga, Pacome Zouzoua ‘Zizzou’ amefunga mabao manne na kuasisti moja katika Ligi Kuu Bara, huku akiwa na mabao matatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na amekuwa gumzo kwa kiwango alichonacho tangu atue na timu hiyo akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Lakini kama unadhani kiwango cha Pacome kimefikia kileleni, umekosea, kwani jamaa amesema anatarajia kurudi na moto zaidi Ligi Kuu Bara ikirejea kutoka kwenye mapumziko ya kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi na Fainali za Afcon 2023 zinazoanza wikiendi hii.
Pacome aliliambia Mwanaspoti kuwa, kitendo cha kupewa muda wa kupumzika kumempa nafasi ya kujiweka vyema zaidi, kwani tangu alipomaliza msimu uliopita akiwa na Asec na kutwaa ubingwa nayo huku yeye akichaguliwa Mchezaji Bora wa msimu, alikuwa hajapumzika japo aliuwasha moto kisawasawa.
Nyota huyo alipewa mapumziko maalumu pamoja na wenzake ambao hata hivyo waliitwa na kocha Miguel Gamondi visiwani Zanzibar kwa ajili ya mechi za Mapinduzi, ila kwa bahati mbaya Yanga ilitolewa katika robo fainali na APR kwa mabao 3-1 na sasa timu imebakiwa na michuano mitatu.
Kikosi hicho sasa kimebakiwa na Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kiungo huyo anashika nafasi ya pili kwa idadi ya mabao matatu, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kikiwa na kiporo dhidi ya Hunsung ya Njombe.
Kiungo huyo alisema mapumziko aliyopewa na benchi la ufundi yamempa fursa ya kurudisha nguvu mwilini na kumfanya ajipange upya kabla ya kureja uwanjani, kwani alikuwa hajapata fursa hiyo.
Staa huyo alisema tangu alipokuwa Asec msimu uliopita alicheza mechi nyingi na walipomaliza msimu akaunga Yanga moja kwa moja bila ya kupata mapumziko.
“Mapumziko ambayo kocha amenipa yatarudisha nguvu kubwa, kiukweli nilihitaji muda wa kutosha kupumzika na kama nisingepata, ingeweza kuathiri ufanisi wangu,” alisema.
Alizungumzia pia homa anayoipata linapokuja suala la kuwania namba ndani ya kikosi hicho, hali inayomfanya ajipange zaidi ili kuhakikisha anatumia vyema kila nafasi anayopata.
“Ushindani wa namba uliopo Yanga unamweka kila mchezaji kwenye presha ya kuhakikisha akipewa nafasi anaitendea haki, ukizubaa utajikuta unasota benchini.”